YANGA KIMENUKA, MMMOJA ANG'ATUKA


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Sarh Ramadhan aliyeamua kubwaga Manyanga
HALI ndani ya uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga, imekuwa tete baada ya baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji, kutaka kuachia ngazi kutokana na mgawanyiko na mwingiliano wa majukumu, hivyo mambo kwenda ndivyo sivyo.
Habari ambazo ziliifikia Sayari jana, zilidokeza kuwa, mwingiliano wa majukumu kati ya kamati moja na nyingine, kumeleta mvurugano mkubwa huku nyingine zikionekana kama muhimu zaidi ya nyingine, hivyo kukosekana kwa umoja katika kuiletea klabu hiyo maendeleo.
Taarifa za awali, zilisema kuwa ndani ya kamati ya Utendaji kumekuwepo na msigano, ikielezwa ndicho kisa baadhi ya mambo kutokwenda vizuri, likiwemo la kuchezeshwa kimakosa kwa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mechi ya Coastal Union.
Licha ya kutakiwa kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu baada ya kulimwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kosa la kumpiga mwamuzi Israel Nkongo katika mechi dhidi ya Azam, alicheza mechi hiyo na Yanga kupokwa pointi tatu na mabao matatu, wakapoteza nguvu ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
Kati ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao wanataka kubwaga manyanga wakikerwa na uendeshaji wa mambo katika klabu hiyo, ni Sarah Ramadhani kwa hoja ya kutothaminiwa kwa mchango wao.
“Nani amekwambia jambo hilo….ninyi hamna dogo, ingawa ni kweli tena mmojawapo ni mimi na wengine, lakini ni mapema mno. Ninataka kufanya hivyo kwa sababu naona kama sina lolote ninalofanya kwa klabu yangu,” alisema Sarah.
Mjumbe huyo, alisema anataka kujiengua kutokana na kunyimwa nafasi ya kutimiza wajibu wake kulingana na nafasi yake, hivyo ni heri ajiweke kando kwa heshima ya wanachama waliompa kura katika uchaguzi wa Julai 18, 2010.
Alisema, akiwa mdau wa kweli wa michezo, anasikitishwa namna mambo yalivyo katika klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wao Nchunga, mojawapo ni kutokuwepo kwa umoja na mshikamano, hivyo kuvuja kwa mipango ya Kamati ya Utendaji.
“Kuna mambo yananiumiza sana, likiwemo la mwingiliano wa majukumu, hivyo kuleta mkanganyiko wa kiutendaji…ni heri nikae kando kuwapisha wengine watakaoweza kuikubali hali hii,” alisema.
Mbali ya Sarah, mjumbe mwingine wa Kamati ya Utendaji (jina tunalo), ameidokeza Sayari kuwa naye yu mbioni kuachia ngazi akichoshwa na kasumba ya viongozi kuingilia masuala yasiyowahusu.
Akitoa mfano hai wa hilo, kiongozi huyo alisema hata kuchezeshwa kwa Cannavaro, ni shinikizo la baadhi ya viongozi wa juu kwani hata Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic, awali hakuwa amempanga akijua anatumikia adhabu.
“Ukweli ni kwamba, viongozi walimlazimisha Papic kumpanga Cannavaro, naye akaona hana jinsi, akampanga na matokeo yake, Yanga imepoteza ubingwa kwa makosa ya kizembe kabisa,” alisema.
Alisema kitendo cha uongozi wa juu kukata rufaa kwa makosa ya wazi yaliyofanywa kwa Cannavaro, ni kama kuwahadaa wanachama kwa sababu kwa mazingira ya jambo hilo, ni maamuzi sahihi kwa mujibu wa kanuni za soka.
Mjumbe huyo alisema, fedha zilizopotezwa kwa kukata rufaa kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni kama zimepotezwa bure kwani zingeweza kufanya kazi nyingine za maendeleo ya klabu.
Kwa Yanga kupokwa ushindi wa Coastal union, wamebaki na pointi 43, hivyo kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wala nafasi ya pili kwani uwezo wake ni kuishia pointi 52 kama watashinda mechi zote tatu zilizobaki dhidi ya Polisi Dodoma, JKT Oljoro na Simba.
Wakati uwezo wa Yanga ni pointi hizo, mtani wake anayeongoza ligi hiyo kwa pointi 56, ataweza kumaliza ligi akiwa na pointi 62, kama atashinda dhidi ya Moro United na Yanga.
Hadi sasa, Azam FC wapo nafasi nzuri ya kuitwaa nafasi ya pili kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake Juni 24, 2007, kwani wakiwa na pointi 50, watamaliza ligi wakigota 59, kama watashinda dhidi ya Mtibwa Sugar, Toto African na Kagera Sugar.
Mwenyekiti wa Matawi ya klabu hiyo, jijini Dar es Salaam, Msumi, amesema kutokana na hali ya mambo yanavyokwenda hovyo ndani ya klabu hiyo, uongozi wa Nchunga, hauna budi kuachia ngazi.
Akizungumza kwa njia ya simu jana jioni, Msumi alisema kuna haja ya Nchunga kuchukua hatua hiyo kwa mustakabali wa Yanga kwa sababu ameshindwa kuongoza kwani tangu alipoingia madarakani, klabu hiyo imekuwa ikiyumba.
Alisema, tatizo la Nchunga, ni kuendesha klabu hiyo bila kufuata katiba, akiweka kapuni hata mikutano ya kikatiba, hivyo klabu kuendeshwa kama shamba lisilo na mwenyewe, ikiwemo baadhi ya watendaji kuteuliwa kienyeji, bila ridhaa ya wanachama.
Juhudi za kumpata Nchunga kutolea ufafanuzi zaidi juu ya masuala yanayoelekezwa kwa uongozi wake, zilikwama baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani.
CHANZO:GAZETI LA SAYARI
                                                

Comments