YANGA HALI MBAYA KIFEDHA, WAANZA KUWEKANA BONDI


DEREVA wa gari la wachezaji wa Yanga, Hafidh Suleiman amezuiwa kwa muda mkoani Arusha kutokana na uongozi wa klabu hiyo kushindwa kulipa deni la hoteli waliyofikia.

Tukio hilo kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika ndani ya Yanga lilitokea juzi wakati wachezaji wa Yanga na baadhi ya viongozi walioambatana na timu hiyo wakijiandaa kuondoka kwenye hoteli waliyofikia iitwayo Joshimel mkoani Arusha.

Yanga ilikuwa mjini humo kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro iliyofanyika Jumatano Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.

“Ilikuwa kama sinema vile, wachezaji wanajiandaa kuondoka wakaambiwa wasitoke kwani hoteli ilikuwa haijalipiwa na uongozi, hivyo wanatakiwa wabaki.

“Tukio la kutaka kuzuiwa wachezaji lilionekana kama lingeleta kizaazaa, hivyo uongozi ukachukua uamuzi wa kumbakisha Hafidh ili kunusuru wachezaji wasizuiwe kuondoka, hilo lilipofanyika ndipo timu ikaruhusiwa kuondoka, maana Hafidh alibaki kama uthibitisho
kuwa fedha zitalipwa,” kilisema chanzo chetu.

Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga alipoulizwa juu ya habari hizo jana alikiri Hafidhi kubaki,
lakini si kwa sababu wameshindwa kulipa deni, ila ni suala la malipo ya hundi wenye hoteli kukataa.

“Siyo kwamba tumeshindwa kulipa deni, sisi huwa tunalipa kwa hundi, kuna sehemu wanakubali hundi na wengine wanakataa, sasa jana (juzi) hao watu wa hoteli tuliwapa hundi wakakataa, maana tulishindwa kwenda benki kutoa fedha kwa sababu jana (juzi) ilikuwa
mapumziko.

“Tukasubiri mpaka leo (jana) ndiyo tumeenda kutoa fedha na kurekebisha hilo jambo na ndiyo
maana tulimuacha Hafidh ili timu iweze kuondoka na leo (jana) tulituma hizo fedha kwake na amezilipa na kesho (leo) atarudi Dar es Salaam, “ alisema Nchunga jana.

Lakini kwa upande wake Hafidh alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo alikana kubaki Arusha kwa sababu ya deni la Yanga na kwamba alikuwa na mambo yake binafsi mjini humo.

Hata hivyo alipobanwa kwamba viongozi wa Yanga wamekiri yeye alibaki Arusha kwa sababu ya uongozi kuchelewa kulipia deni la hoteli, Hafidh alisema: “Hapana, nilikuwa na mambo yangu Arusha, hayo unayosema hayapo, ila kama viongozi wamesema kweli hivyo, labda inawezekana.”

CHANZO:GAZETI LA HABARI LEO
 

Comments