YANGA BADO YAWEWESEKA NA MAAMUZI YA TIBAIGANA


SIKU moja baada ya kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka  Tanzania (TFF) kutupilia mbali rufaa ya timu ya Yanga kupinga kupokwa pointi tatu na mabao matatu, uongozi wa klabu hiyo umesema bado unatafakari cha kufanya. 
Kamati ya nidhamu chini Mwenyekiti wake kamishna mstaafu wa Polisi Alfred Tibaigana iliyokutana juzi ilitupilia mbali rufani hiyo ya Yanga iliyowasilishwa na Yanga ikilalamikia kamati ya  kamati ya Ligi kuipoka pointi hizo na mabao matatu baada ya kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alikuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi tatu. 
Ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kwamba wamezipata taarifa za rufaa yao kutupiliwa mbali lakini kwa sasa wanaendelea na mambo mengine kwanza ambayo yana manufaa na klabu hiyo huku wakiliweka kiporo suala hilo. 
Alisema kwa sasa viongozi wengi wa klabu hiyo wapo nje ya jiji la Dar es Salaam kwa majukumu tofauti lakini bado kuna nafasi ya kukata rufaa kwa kamati ya Rufaa kama itabidi kuwa hivyo kwa kuwa muda bado upo. 
“Tumepata taarifa za rufaa yetu kushindwa, hivyo ni mapema mno kutoa uamuzi tutkaochukua baada ya hatua hiyo, kwa sasa tunaendelea kuchapa kazi kwanza,”alisema Sendeu. 
Aprili 2 mwaka huu Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha Cannavaro  kwenye mechi ya Ligi Kuu bara kati ya timu hizo iliyofanyika Machi 31 mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura  Yanga katika rufani hiyo iliwasilisha sababu nane za kupinga kupokwa pointi hizo,  kubwa zikiwa Cannavaro hakustahili kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, si aliyempiga refa Israel Nkongo, ripoti za refa na kamishna wa mechi yao dhidi ya Azam zilionesha dalili ya njama (conspiracy) kwani zilifanana.

“Pia Cannavaro alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao adhabu zao zilisimamishwa na Tibaigana, hivyo katika  uamuzi wake, Kamati imesema adhabu ya Cannavaro ya kukosa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom ilitolewa na refa na si Kamati ya Ligi kama ambavyo inalalamikiwa na Yanga, na kanuni hiyo haikatiwi rufani”, alisema Wambura. 
Wambura aliongeza kuwa barua ambayo TFF iliiandikia Yanga kuhusu adhabu ya mchezaji huyo ilikuwa wazi kwani ilikariri kanuni ya 25(c), hivyo kitendo cha kumtumia mchezaji huyo ulikuwa ni uzembe wa kutoheshimu kanuni na kama haikufahamu vizuri kanuni hiyo ilikuwa na fursa ya kuiandikia TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 25(f) ili kupata ufafanuzi kabla ya kuamua kumtumia mchezaji huyo. 
“Vilevile adhabu zilizokuwa zimesimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ni zile ambazo zilikuwa zimetolewa na Kamati ya Ligi, na si zile zilizotolewa uwanjani na refa na kuhusu madai ya conspiracy kwa ripoti za kamishna wa mchezo huo na refa, Kamati imebaini kuwa hazifanani, na suala lililokuwa likibishaniwa (contentious issue) lilikuwa ni kunyang’anywa pointi tatu,”aliongeza Wambura. 
Aidha, wambura alisema kuwa Kamati ilikariri Ibara ya 50 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuwa mchezaji anayembughudhi refa kwa njia yoyote ile anastahili kufungiwa kwa angalau mechi sita.
mwisho 

Comments