WIGAN WAIKALISHA ARSENAL EMIRATES

MABAO ya mapema ya Franco di Santo na Jordi Gomez, yameiwezesha Wigan kujitoa kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya kuvuna ushindi wa kwanza kihistoria mbele ya Arsenal usiku huu Uwanja wa Emirates.
Hadi mapumziko, tayari Arsenal ilikuwa imekwishalowa 2-1, mabao ya Wigan yakitiwa kimiani na Di Santo dakika ya saba na Gomez dakika ya nane.
Mabao ya hayo ya haraka haraka ya Wigan yaliwachanganya Arsenal na iliwachukua dakika 12 kukombo moja, likitiwa kimiani na Thomas Vermaelen dakika ya 21.
Pamoja na kipigo hicho, The Gunners wanabaki nafasi ya tatu kwenye msimamowa Ligi Kuu, kwa pointi zao 64, baada ya kucheza mechi 34.
Ikiwa katika nafasi ya nne, Tottenham ndio timu inayoitia jakamoyo Arsenal katika kinyang’anyiro cha nafasi ya tatu, kwani imecheza mechi 33 na ina pointi 59.
Wigan sasa iko nafasi ya 16 na kujitoa kwenye eneo la hatari, baada ya kufikisha pointi 34 katika mechi 34, ambayo ni sawa na wastani wa pointi moja kila mechi iliyocheza.
QPR imeshuka hadi nafasi ya 17, ikiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 34, wakati Bolton inabaki nafasi ya 18 kwa pointi zake 29 kwenye mechi 32, Blackburn pia inabaki nafasi ya 19 kwa pointi zake 28 kwenye mechi 34, wakati  Wolves inaendelea kuzibeba timu nyingine zote 19 katika ligi kwa pointi zake 23, kwenye mechi 34.

Comments