WATANZANIA KUCHEZESHA AFRIKA KUSINI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi wane wa Tanzania kuchezesha mechi ya marudiano ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Black Leopards ya Afrika Kusini na Warri Wolves ya Nigeria itakayochezwa nchini Afrika Kusini kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
Waamuzi hao ni Waziri Sheha atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake watakuwa John Kanyenye na Erasmo Jesse. Mwamuzi wa akiba (fourth official) atakuwa Israel Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Aurelio Mathias wa Msumbiji.
Mechi ya kwanza kati ya timu hizo itachezwa Jumapili (Aprili 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Warri City ulioko Jimbo la Delta nchini Nigeria na itachezeshwa na waamuzi kutoka Senegal wakati Kamishna atakuwa Inyangi Bokinda wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Comments