WASHINDI WA TUZO ZA KILI KUSHUKURU MIKOANI

Meneja wa bia ya Kilimanjaro George Kavishe akifafanua jambo kuhusiana na ziara hiyo, kushoto ni mshindi wa Tuzo tatu, Diamond.
WASANII walioshinda tuzo za muziki za Kili mwaka 2012 pamoja na wale waliokuwa wakiwania tuzo hizo wanatarajiwa kufanya ziara maalum katika mikoa sita ili kutoa shukrani kwa mashabiki sambamba na kuwapa burudani.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) George Kavishe alisema kwamba lengo la ziara hiyo pia ni kuwapa fursa mashabiki wa sehemu husika kuwashuhudia wasanii hao kwa njia ya burudani.
Alisema katika mikoa ambayo wasanii hao watapita kutaendeshwa zoezi la kuwapata wasanii chipukizi ambapo kila mkoa utatoa msanii mmoja ambaye baadaye atakuja jijini Dar es Salaam kurekodi na mmoja ya wasanii maarufu.
Alisema mchakato wa kuwapata wasanii hao chipukizi utaendeshwa katika tarehe maalum zilizopangwa katika kila mkoa husika huku majaji wakitarajiwa kuwa wasanii wa muziki wa bongo fleva wakiwemo Profesa J, Juma Nature na Queen Darleen.
Kavishe aliongeza kuwa ziara hiyo inatarajiwa kuanza Aprili 28 mkoani Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri, wakati Mei 7 itakuwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kilimanjaro itakuwa Mei 12 kwenye Uwanja wa Ushirika na Mbeya itakuwa Mei 19 katika Uwanja wa Sokoine.
Aidha wakazi wa Mtwara watapata fursa hiyo Mei 26 katika uwanja wa Mtwara kabla ya ziara hiyo kuhitimishwa Juni 2 kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar salaam.
Baadhi ya wasanii watakaoshiriki katia ziara hizo ni pamoja na Diamond, Isha Mashauzi, Ali Kiba, At, bendi ya Twanga Pepeta, Ben Pol, Kalidjo Kitokololo, Ommy Dimples, Khadija Kopa, Suma Lee, Jaguar, Barnaba, Warriours from the East, Queen Darlin na wengineo.
Kwa upande wake msanii aliyefanikiwa kutwaa tuzo tatu mwaka huu Nassib Abdul ‘Diamond’ akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake pamoja na kushukuru kwa mashabuiki kumuwezesha kutwaa tuzo hizo, aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo watapita kufanya maonyesho.

Comments