WASANII WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUJIKWAMUA


Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini Bw. Adrian Nyangamale (Kulia) akizungumza na wadau wa Jukwaa la Sanaa wakati akiwasilisha mada iliyohusu Sanaa ya Uchongaji na Mchango wake katika sekta ya Utalii nchini.Kulia ni Afisa Sanaa wa BASATA Bw. Malimi Mashili.
     Afisa wa Sanaa kutoka BASATA Bw. Mashili akisisitiza jambo wakati akihitimisha Jukwaa la Sanaa wiki hii.
 Mkurugenzi wa Kundi la Parapanda Art Theatre Bw. Mgunga Mwamnyenyelwa akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu maendelea ya tasnia ya Sanaa nchini huku akisikilizwa na sehemu ya wadau wa Sanaa. Alieleza kuwa, Tanzania ni nchi ya kwanza kuwa na sera ya Utamaduni katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkongwe wa Sanaa za Maonesho nchini ambaye pia ni mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Mzee Nkwama Bhallanga akichangia mada kwa umakini kwenye Jukwaa la Sanaa. 
Na Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wametakiwa kutoitegemea Serikali kwa kila kitu na badala yake waweke mikakati yao katika kutumia fursa zilizopo ili kujikwamua na changamoto zinazowakabili.
Wito huo umetolewa wiki hii na Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa za Maonesho la Parapanda Arts Theatre Bw. Mgunga Mwamnyenyelwa wakati akichangia mada iliyohusu Sanaa ya Uchongaji na Mchango wake katika sekta ya Utalii nchini kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, pamoja na changamoto zilizopo, Serikali imejitahidi kuweka miundombinu, sera na taratibu mbalimbali za kuongoza sekta ya Sanaa hivyo wasanii hawana budi kutumia fursa hizo katika kujiletea maendeleo na kumaliza matatizo yanayowakabili.
“Wasanii tuache kulalamika, tujipange katika kutumia fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na kushirikisha wasomi mbalimbali. Nchi yetu imeweka mazingira mazuri ya kukuza sekta ya sanaa hivyo tuyatumie” alisisitiza Mgunga.
Aliyataja baadhi ya mazingira hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo mbalimbali vya Sanaa kama vya Bagamoyo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Butimba na vinginevyo ambavyo vinatosha kuzalisha wataalam wa Sanaa na wasanii wenye weledi.
Aidha, aliongeza kuwa nchi ya Tanzania ni ya kwanza kuwa na sera ya utamaduni ikilinganishwa na nchi zingine za ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumeenda Kenya,Ethiopia na Uganda, nchi ya Tannzania inaongoza kwa kuwa na vyuo vingi vya Sanaa lakini pia ni ya kwanza kuwa na Sera ya Utamaduni” aliongeza Mgunga.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania Bw. Adrian Nyangamale alisema kuwa, shirikisho lake limejipanga kukuza sanaa za ufundi ili kuweza kuwakomboa wasanii na hatimaye kufikia kiwango cha kimataifa.
“Shirikisho limejipanga kuwa na jumba kubwa la Sanaa za ufundi, vituo vya mikoa vya sanaa, kukuza soko la ndani na nje ikiwa ni pamoja na kuunda chombo cha kuratibu na kudhibiti uuzaji holela wa kazi za wasanii” aliongea Nyangamale. 

Comments