WABUNIFU WA MAVAZI NA MITINDO WAOMBOLEZA KIFO CHA KANUMBA


Siku chache baada ya kutokea kifo cha msanii nguli na mwanzilishi wa Bongo Movies Marehemu Steven Kanumba; Tasnia ya mitindo imeelezea ni kwa jinsi gani imeshtushwa na kusikitishwa na kifo cha nguli huyo wa filamu si tu nchini Tanzania bali Afrika kwa ujumla wake. 
Marehemu Steven Kanumba alikuwa na mchango mkubwa sana katika kuendeleza si tu Sanaa ya maigizo, bali pia Ubunifu wa mitindo kwa kuhudhuria maonyesho mbalimbali ya mitindo ya mavazi Tanzania kama Swahili Fashion Week, Red Ribbon Fashion Gala, Lady In Red na kadhalika. 
Akimzungumzia marehemu Steven Kanumba kwa niaba ya Tasnia ya Ubunifu wa mavazi, mbunifu nguli wa mavazi Afrika Mashariki na Kati Mustafa Hassanali alisema “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi, Kanumba ameondoka katika kipindi ambacho taifa linauhitaji mchango wake san. Ni majonzi mazito si tu kwa tasnia ya filamu bali pia kwa tasnia ya ubunifu wa mitindo, kwani Kanumba alijikita katika kutangaza mavazi yaliyobuniwa na wabunifu wa hapa nyumbani, hakuwa balozi wa filamu tu bali pia balozi wa mitindo Tanzania 
“Kanumba ni kijana thabiti aliyekuwa akisimamia ukweli, uwazi, uwajibikaji na kile alichokiamini kuwa ni haki. Ama kwa hakika atakumbukwa kwa mengi na pengo lake halitaweza kuzibika”. Aliongeza Hassanali. 
Tasnia nzima ya ubunifu wa mitindo inasikitika sana kuondokewa na mpendwa wetu Ndugu Steven Kanumba na inatoa pole za dhati kwa ndugu, jamaa, marafiki, wanafilamu, mashabiki wake na watanzania wote kwa ujumla. Tulimpenda sana ila Mwenyezi Mungu kampenda zaidi, na kazi yake siku zote haina makosa. Pumzika kwa Amani. Amin

Comments