UONGOZI YANGA WAWAPOZA MASHABIKI WAKE


LICHA ya kutakiwa kujiweka kando kwenye uongozi baada ya timu kufanya vibaya katika ligi kuu soka Tanzania bara, uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umewaomba wanachana kuwa na subira mpaka ligi itakapomalizika. 
Hatua hiyo inafuatia wanachama wa klabu hiyo kuutaka uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga ujiuzulu baada ya timu kupoteza mwelekeo kwenye ligi hiyo na hatimaye kushindwa kutetea ubingwa wake. 
Katibu mkuu wa Yanga Selestine Mwesiga ameiambia mamapipiro blog kwamba, kujiuzulu kwa viongozi si suluhisho la timu kufanya vibaya kwenye ligi hiyo ambayo inaelekea ukingoni. 
Alisema kufanya vibaya kwa timu hiyo huenda kunachangiwa na mambo tofauti hivyo kuuutupia lawama uongozi kujiondoa madarakani si suluhisho hivyo ligi itakapomalizika watakaa na kujua tatizo ni nini. 
“Unajua kuteleza kuna sababu nyingi labda tatizo ni katika idara ya ufundi, ama utawala na hata mfumo mzima wa ligi sasa kutaka uongozi kujiuzulu haiwezi kusaidia lolote, kikubwa ni kusubiri ligi imalizike kwanza,”alisema. 
“Si utamaduni wetu kujiuzulu wakati ligi haijaisha, tunajua wapenzi wetu wanaumia sana kutokana na timu kufanya vibaya lakini nawaomba wanachama wawe na subira na tutahakikisha timu inafanya vema katika michezo yake iliyosalia kwenye ligi,”alisema Katibu huyo. 
Katibu huyo aliongeza kwamba wanachama wa Yanga wanahaki ya kulalamika mwenendo mzima wa timu hiyo kwani ni wajibu wao lakini wanapaswa kukumbuka kuwa uongozi huohuo muda mfupi baada ya kuingia madarakani timu yake ilitwaa mataji matatu.

Comments