UCHUNGUZI WA AWALI WAONYESHA POMBE KALI ILICHANGIA KIFO CHA KANUMBA


Jakaya akihani wafiwa
POMBE kali (Whisky) aina ya Jacky Daniel, imetajwa kama chanzo cha kifo cha mwigizaji nyota wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba aliyefariki usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake, Sinza, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela amesema leo kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha hivyo, lakini bado wanaendelea na uchunguzi zaidi, ili kujua zaidi.
ACP Kenyela amesema kwamba Kanumba wamefanikiwa kumuhoji mtuhumiwa wa kwanza katika tukio hilo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na katika maelelezo yake amekanusha kumsukuma Kanumba.
Vyombo vingi vya habari vilimnukuu ndugu wa Kanumba, Sethi jana akisema kwamba Lulu alimsukuma mwigizaji mwenzake huyo katika ugomvi wao wa wivu wa kimapenzi hadi akaanguka na kufariki dunia.
Akizungumza kutokana na maelezo ya Lulu, Kamanda huyo alisema kwamba; ugomvi wao ulitokana na Kanumba kutaka kumdhibiti Lulu wakati akizungumza na simu.
“Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti, akitaka aelezwe kwa nini alitoka nje kupokea simu, huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.
Baada ya Lulu kuona Kanumba anamfuata, aliamua kukimbia kutoka nje ya geti, lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba  alimkamata na kumrudishwa ndani. Kanumba akiwa amemshikilia, waliingia wote chumbani na kufunga mlango. Sasa haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu, anadai kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba,”alisema Kamanda huyo.
Akiendelea kumnukuu Lulu, Kamanda huyo anasema; “Baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini,”alisema.
Alisema uchunguzi wa tukio zima ukikamilika, hatua inayofuata ni kumpeleka Lulu mahakamani kama mtuhumiwa wa mauaji.
Wakati huo huo: mchana wa leo, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alifika nyumbani kwa marehemu, Sinza Vatican kuhani msiba.
Mama wa marehemu anatarajiwa kuwasili leo- ili kwa pamoja na Kamati ya Mazishi waamue kuhusu mwili wa marehemu uzikwe wapi.
Kamati ya Mazishi, inataka kumshawishi mama huyo anayetokea Bukoba, akubali Kanumba azikwe Dar es Salaam.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa Jumanne katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam na baada ya hapo ndipo litafuatia zoezi la mazishi.
HISTORIA YAKE:
Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, mwaka 1984, mkoani Shinyanga, kabla ya umauti kumfika Aprili 6, mwaka 2012.
Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Ni wakati huo akiwa Jitegemee, Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.
Hivi karibuni, alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
Nigeria sasa wanajua Tanzania kuna filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri ya Kanumba.
Mwenyewe aliwahi kukaririwa alifika hadi Hollywood, Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.

Comments

  1. YANGA BOMBA - UHURU BRANCHApril 8, 2012 at 9:03 PM

    kumbe alikua anakunywa pombe!!si mara kadhaa alikua akidai hanywi huyu au alikua akinywa akiwa na kazi maalum?

    kweli huu msiba utafunua mambo mengi.

    Otherwise,Poleni sana wafiwa

    mdau wa bomba,revere,massachussetts,usa

    ReplyDelete

Post a Comment