UBAO WA MATANGAZO TOKA TFF,YALIYOJIRI MKUTANO MKUU


  
EL MAAMRY, NDOLANGA WATUNUKIWA URAIS WA HESHIMA
AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa TFF, Alhaji Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga. 
Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji Ndolanga aliongoza FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004. 
BAJETI YA MWAKA 2012
Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya matumizi ya TFF ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh. 7,572,991,433 kupitia vyanzo mbalimbali. 
Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuingiza asilimia 22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali, misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja vinatarajiwa kuingiza asilimia nne ya mapato yote. 
UUZWAJI WA TIMU
Uuzaji wa timu linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF imeweka utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe uuzaji, na timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika. 
MFUMO WA MASHINDANO
Kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali inayosababisha baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi ya moja katika msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya. 
Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika mpira wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya miaka mitatu ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa ligi, na kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani. 
Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa. Kwa sababu TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni wanachama wa federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi, kwa vile TFF haiwezi kusimamia ligi zote. 
MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika maeneo mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano. 
Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi na moja za sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuongeza mikoa mipya ya kijiografia. 
Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara, Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam, Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na Pwani/Morogoro. 
Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda. 
HESABU ZILIZOKAGULIWA
Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010 (Audited Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC Associates kuwa mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo.  
KANUNI ZA NIDHAMU, MAHAKAMA YA USULUHISHI
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Tenga aliwaambia wajumbe kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji wa Mahakama ya Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa chombo cha juu cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika mwaka huu. 
Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za Taifa za vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika nyanja mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na kutengeneza mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali kumalizika mwaka huu. 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments