TUTAWADUNDA NA BARIDI LAO- MILOVAN


Simba wakiwa Setif

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema hali ya hewa ya mji wa Setif ambayo ni baridi kali inaweza kuwa faida kwa timu yake na si hasara.
Akizungumza na tovuti ya Simba, Milovan alisema hali ya hewa ya baridi huwafanya wachezaji wasichoke mapema tofauti na joto ambalo huchosha.
Kuna baridi za aina mbili. Kuna baridi inayotokana na hali ya hewa ya mahali na kuna baridi inayotokana na eneo kuwa kwenye miinuko (altitude). Zote ni baridi lakini zina tofauti.
“Ile ya miinuko huwafanya wachezaji washindwe kupumua vizuri na huwa na athari mbaya sana. Tuliliona hili kwenye mechi ya Kiyovu lakini hapa Setif hakuna miinuko sana kama Rwanda na hivyo watu wanaweza kucheza vizuri,”alisema.
Alisema jambo la muhimu kwa timu yake ni kutoathiriwa na sauti za washangiliaji wa Setif wala kughadhabika kirahisi wanapochokozwa na wapinzani wao.
“Mechi yetu na Setif ni ngumu sana. Kila timu ina nafasi ya kufanya vizuri ingawa sisi tuna faida kutokana na ushindi tulioupata nyumbani. Ni jukumu letu kuhakikisha tunaulinda ushindi wetu,” alisema.
Simba leo imefanya mazoezi katika Uwanja wa Mei 8, 1945, ambao utatumika kwa mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF) baina ya Wekundu wa Msimba na ES Setif ya Algeria.
Mazoezi hayo yalikuwa ya kwanza kufanywa na Simba katika mji huu wa milima milima na hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali kwa kiwango cha nyuzijoto tisa.
Simba walianza mazoezi katika uwanja huo majira ya saa 12:30 kwa saa za hapa sawa na saa mbili na nusu usiku huko, na mazoezi hayo yalifanyika kwa muda wa masaa mawili na nusu.
Wachezaji wote wa Simba walihudhuria mazoezi hayo ambayo kama kawaida yalikuwa chini ya uangalizi wa benchi la ufundi na yalihudhuriwa na Watanzania waliokuja kuisapoti timu, wananchi wa Setif na askari waliokuwa wakiangalia mazoezi hayo na kulinda usalama.
Kabla ya Simba kufanya mazoezi, uwanja huo ulitumiwa na timu ya Setif kwa mazoezi pia na ilibidi wachezaji wa Simba wasubiri nje ya uwanja kwa takribani dakika 45, kabla ya kuruhusiwa kuingia.

Comments