TERRY: TUTAMALIZA BIASHARA CAMP NOU


Shujaa Drogba

BEKI la kati, John Terry amesema anajiamini Chelsea itatinga Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Barcelona 1-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge katika Nusu Fainali ya kwanza usiku wa jana.
Bao la Drogba mwishoni mwa kipindi cha kwanza lilitosha kuipa timu ya London ushindi na Nahodha huyo Chelsea anaipongeza timu yake kwa jitihada kubwa walizoonyesha kwenye mechi na Barcelona.
“Nafikiri tulitulia usiku huu (jana), tulizidiwa kumiliki mpira mwanzoni, sifikiri kama tuliugusa katika dakika 10 hadi 15 za mwanzo,” alisema Terry katika taarifa iliyoifikia bongostaz.
“Kawaida wao ni timu babu kubwa. Tulitakiwa kutulia haswa. Ilikuwa babu kubwa, kujituma kwa kila mmoja bila kuchoka.”
Licha ya bao la Drogba, lakini wageni walipoteza nafasi zaidi ya tatu za wazi za kufunga na Terry amempongeza sana Nahodha wa Ivory Coast kwa bao lake.
“Ni hodari, ndivyo anavyokuwa katika mechi kuvwa kama hizi, ulimuona Jumapili dhidi ya Tottenham Uwanja wa Wembley,”alisema Terry.
“Anakabiliana na mabeki bora duniani na anawaacha. Kuna wakati alipagwa, lakini aliimudu mechi vizuri.”
Chelsea sasa itasafiri hadi Uwanja wa Camp Nou wiki ijayo huku Nahodha wake, akiwa mwenye kujiamini kwamba watacheza fainali msimu huu dhidi ya ama Real Madrid au Bayern Munich.
“Nafikiri dhahiri itakuwa mechi ngumu huko, tuliokoa mabao kadhaa ya wazi kwenye mstari wa lango letu, dhahiri watapata nafasi huko kwenye Uwanja wenye eneo kubwa la kuchezea, wao ni wazuri,”alisema.
“Tumeonyesha tunawaheshimu usiku huu (jana), lakini hatuko kwenye himaya yao na tutafanya biashara.”
Drogba, wakati huo huo amesema anafikiri The Blues wamejifunza kutokana na mwaka 2009 walipotolewa na Barcelona na amefurahishwa na matokeo ya jana.
“Nafikiri tumejifunza [kutokana na makosa ya kufungwa 2009]. Tumeimarika ndani ya miaka mitatu, kwa sababu hatukufungwa bao (la nyumbani),” alisema.
“Tuna furaha na matokeo haya. Ni mazuri, 1-0 nyumbani, ni matokeo mazuri. Tutakwenda huko na kujaribu kufunga bao lingine na kufuzu,”amesema Drogba kama tunavyomnukuu bongostaz.blogspot.com.

Comments