TASWA WAOMBOLEZA KIFO CHA KANUMBA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MSIBA WA KANUMBA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinaungana na wasanii wote nchini na Watanzania kwa ujumla kuombeleza kifo cha msanii mahiri Steven Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi jijini Dar es Salaam.
TASWA imeshtushwa taarifa za kifo cha Kanumba, hivyo tunatoa pole kwa familia ya msanii huyo na wasanii wote wengine katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na msanii huyo. Kanumba atakumbukwa na waandishi wa habari za michezo na burudani kutokana na ukaribu wake kwao na alikuwa na ushirikiano wa kutosha pale alipoombwa kufanya hivyo, hali ambayo waandishi wa habari za michezo na burudani nchini wataendelea kumbukumbuka.Mungu amuweke mahali pema peponi.
B.PONGEZI KWA SIMBA KUINGIA 16 BORA
TASWA inatoa pongezi za dhati kwa timu ya Simba ya Dar es Salaam baada ya kufanikiwa kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuitoa ES Setif ya Algeria Ijumaa iliyopita.
Tunaamini kusonga mbele kwa Simba ni hatua nzuri katika kufikia mafanikio ya kweli ya mpira wa miguu hapa nchini, hivyo tunaamini kila mdau wa soka atakuwa ameguswa kwa namna moja au nyingine kutokana na mafanikio ya Simba.
Tunawasihi wachezaji wa Simba na viongozi pamoja na mashabiki wa klabu hiyo, wasibweteke na mafanikio hayo badala yake waunganishe nguvu ili waingie hatua inayofuata hatimaye watwae ubingwa maana hakuna lisilowezekana chini ya jua.
WAANDISHI WALIOSHINDA TUZO
Kamati ya Utendaji ya TASWA inatoa pongezi za dhati kwa waandishi wa habari za michezo walioshinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) zilizofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Waandishi hao ni Imani Mani aliyeshinda upande wa magazeti, Anwar Mkama upande wa televisheni na Abdallah Majura upande wa redio, ambao tunaamini juhudi za kazi zao zimefanikisha kupata tuzo hizo.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
08/04/2012           




Comments