TANGA CEMENT WAIKABIDHI COASTAL UNION BASI



Na Ahmed Khatib ,Tanga 
TIMU ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ ya jijini hapa, imekabidhiwa basi lenye thamani ya sh milioni 45 na kampuni ya saruji ya Tanga, jana.
Akikabidhi basi hilo kwa viongozi wa Coastal, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement,  Erik Westerberg, alisema, basi hilo wamelitoa kutokana na juhudi zilioneshwa na timu hiyo katika Ligi Kuu ya soka Tnzania Bara inayoelekea ukingoni.
“Msaada huu wa leo, nina imani kuwa utaongeza ari na nguvu ya kujituma zaidi katika michezo iliyobaki, kwani mafaniko yenu ndio mafaniko ya Tanga Cement na tunaahidi kufanya mazuri zaidi, ikiwa na nyie mtaonyesha moyo wa kizalendo kwa timu yenu kufanya vizuri zaidi,” alisema Westerberg.
Hata hivyo, Westerberg, alitoa rai kwa viongozi wa klabu hiyo watambue kuwa, basi hilo ni kwa matumizi ya timu tu na sio mengine binafsi, huku akiwataka kulitunza kwa maendeleo ya timu yao.
Naye Mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Aurora, alisema, msaada kampuni hiyo waliyoutoa, ni wa kwanza katika kipindi hiki na hiyo ni kutokana na kikosi hicho kufanya vizuri katika ligi.
Aurora, aliomba kampuni nyingine zenye moyo wa kizalendo, kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mechi za ligi ijayo, kwani hii ya sasa iko mwishoni.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Said Sued, aliwahakikishia mashabiki wao kuwa, watahakikisha wanabaki nafasi ya nne mwishoni mwa ligi kuu, huku akisisitiza umoja na mshikamo kwa viongozi na wachezaji wenzie, kuwa ndio siri kubwa ya mafanikio.
Timu hiyo, kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Villa Squad utakaochezwa jijini Dar es Salaam wiki hii.

Comments