SIMBA WAMSHANGAA AZIM NA AHADI ZAKE


Azim
UONGOZI wa klabu ya Simba umeshangazwa na taarifa zinazotolewa na aliyewahi  kuwa mfadhili wa timu hiyo, Azim Dewji kuhusiana na kutoa fedha kwa wachezaji wa timu hiyo, sambamba na kuileta timu ya Tp Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) .
Hatua hiyo inafuatia hivi karibuni Dewji kukaririwa na vyombo vya habari kutoa shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuipongeza Simba kutokana na kutinga hatua ya pili ya kombe la Shirikisho Afrika (CAF) baada ya kuitoa Es Setif ya Algeria wiki, pia kuileta TP Mazembe kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na Simba.
Mmoja ya viongozi wa Simba (jina tunalo) amesema leo kuwa Dewji amekuwa akifanya mambo kinyemela hali ambayo inasababisha kuwepo kwa mvurugano usio na maana ndani ya klabu hiyo.
Akifafanua zaidi, kiongozi huyo alisema kuwa hata zile fedha za awali (sh.mil.15) ambazo ilidaiwa kuwa amewapa wachezaji hazikuwa na ukweli wowote kwani fedha hizo zilitolewa na uongozi.
“Nakumbuka Azim alikuja kuongea na wachezaji baada ya mchezo wetu na Es Setif hapa nyumbani na kuahidi kutoa mil.15 lakini hakuzitoa na matokeo yake wachezaji walipomfata alidai kuwa hana fedha mpaka mwisho wa mwezi.
“Hata hivyo Dewji hakutoa hiyo hela na tuliposhinda Algeria alidai atawapa wachezaji Mil.15 pindi watakaporejea, lakini timu imerejea tangu jumatatu na mpaka hii leo (jana) hakuna kitu kama hicho hata taarifa za viongozi kukabidhiwa hizo hela ni uongo mtupu,”Aliongeza.
Aidha kiongozi huyo aliongeza kuwa hata taarifa za Dewji kuileta TP Mazembe kwa ajili ya kuja kuipa makali Simba kabla ya mechi yake ya kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan hawana taarifa nazo zaidi ya kuzisoma tu kwenye magazeti.

Comments