SIMBA SC KUCHEZA USIKU NA MORO TAIFA


MECHI ya Ligi ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Moro United iliyokuwa ichezwe Aprili 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imerudishwa nyuma hadi Jumatatu ya Aprili 23 mwaka huu kwenye uwanja huo huo na itaanza saa 1 kamili usiku.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura amesema kwamba mabadiliko hayo yamefanyika ili kuipa Simba fursa ya kujiandaa vizuri kwa mechi yao ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Alisema pia mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Aprili 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam imesogezwa mbele hadi Aprili 22 mwaka huu kupisha mechi ya U20 kati ya Tanzania na Sudan itakayochezwa Aprili 21 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine mbili zimefanyiwa marekebisho; Coastal Union na Kagera Sugar zilizokuwa zicheze jijini Tanga, Aprili 29 mwaka huu, mechi yao imesogezwa hadi Aprili 30 mwaka huu ili kupisha shughuli za Mei Mosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Nazo Azam na Toto Africans zilizokuwa zicheze Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, sasa zitacheza Aprili 28 mwaka huu.

Comments