QUEEN DARLEEN:DADA WA DIAMOND ALIYETIWA NDIMU NA TUZO YA KILI


“Kwa kupata tuzo hii nimeondoa dhana kwamba wasanii waliokuwa wanashinda walikuwa wanapendelewa,”hiyo ni kauli ya Queen Darleen ambaye alitwaa tuzo ya wimbo bora wa Ragga/Dancehall katika tuzo za Kili mwaka 2012.
“Nimefurahi sana kutwaa tuzo hizi ambazo ni kielelezo cha ubora wa kazi za msanii husika, nawashukuru mashabiki walionipigia kura, lakini napenda kusema kuwa tusipende kukariri hakuna upendeleo wowote,”anasema.
Katika mahojiano mahojiano mamapipiro blog msanii huyu anasema zamani alikuwa akiamini maneno ya watu kuwa tuzo hizo zinatolewa kwa upendeleo na hivyo kumfanya kutokuwa na imani nazo kabisa.
Hata hivyo baada ya usiku huo kufanikiwa kutwaa tuzo hizo ameamua kuachana na dhana hiyo mgando ambayo imejengeka vichwani mwa watu wengi, hivyo kuwataka kuamini kuwa tuzo hizo anapata mtu anayestahili.
Queen Darleen akizungumza na Dina Ismail

Darleen ambaye wimbo wake Maneno Maneno aliomshirikisha Dully Sykes ndiyo umemuwezesha kutwaa tuzo hiyo akizipiku nyimbo za Goog Look wa Ay ft Ms Trinity, Ganjaman wa Dabo, Kudadadeki na Poyoyo za Malfred.
Akiwa na nyimbo mbili tu wa kwanza ukiwa ‘Wajua Nakupenda’ aliomshirikisha Alikiba na Maneno Maneno, tangu ajikite kwenye medani hiyo mwanzoni mwa mwaka 2000, Darleen anasema baada ya kupata tuzo hiyo itabidi aelekeze nguvu zaidi katika muziki huo ambao awali aliufanya kwa kujifurahisha tu.
Anasema ndiyo maana amekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kujikita zaidi katika shughuli zake binafsi na masuala ya kifamilia zaidi kwani niliona kujikita sana kwenye muziki ni kupoteza muda wangu.
“Tuzo hii itanipa nguvu na kuongeza jitihada katika muziki kwani zamani niliona kama napoteza muda nikifanya mambo ya muziki lakini kwa heshima waliyonipa mashabiki sina budi kuwalipa kwa mambo maziri,”anasema.
Msanii huyo anaongeza kuwa wimbo wake huo ni wa pili tangu ajikite kwenye game mwaka 2000 kama aliposhirikishwa na Dully Sykes katika wimbo wake wa ‘Historia ya Kweli’ na wimbo wake wa kwanza 'Wajua Nakupenda' aliutoa mwaka 2006 huku akiendelea kuwa juu mpaka alipotoa Maneno Maneno mwishoni mwa 2011.
HISTORIA YAKE:Jina lake halisi ni Mwajuma Abdul Juma, wakizaliwa baba mmoja mama tofauti na msanii wa bongo fleva Nasib Abdul ‘Diamond’ ambapo alizaliwa jijini Dar es salam mwaka 1985 na kupata elimu yake ya msingi na Sekondari jijini Dar es Salaam.
Amekuwa akiupenda muziki tangu akiwa mdogo ambapo tangu kushirikishwa katika singo hizo ya Dully Sykes jina lake lilishika kasi kwenye medani hiyo na hivyo kuanza kupata mialiko ya kimuziki sambamba na kushirikishwa katika kazi ya baadhi ya wasanii ikiwemo singo ya Mtoto wa Geti Kali ya Inspekta Haroun, hivyo jina lake kubaki kuwa vinywani mwa watu.


 
Hata hivyo mwaka 2005 alijiweka kando na muziki baada ya kujifungua mtoto wa kiume aitwaye Rooney (6), kabla ya kurejea tena jukwaani mwaka 2006 alipotoka na singo yake ya kwanza iitwayo Wajua Nakupenda aliomshirikisha Ali Kiba ambayo pia ilifanikiwa kufanya vema.
Darleen alielekeza nguvu zake katika kutunza familia yake huku muziki akiupa nafasi ndogo kabla ya mwishoni mwa mwaka jana kutoka na singo ya Maneno Maneno aliomshirikisha Dully Sykes ambao ulipata matokeo makubwa na hatimaye kutwaa tuzo hizo.
Anavutiwa zaidi na wasanii kama Chris Brown, Eve kwa upande wa wasanii wa nje ya nchi huku kwa hapa ndani akivutiwa na Rachel wa THT, Diamond, Ali Kiba na Mwasiti.
Queen Darleen anasema atakuwa mchoyo wa fadhila kama asipowashukuru waliomuwezesjha kufika hapo akiwemo meneja wake Guru ramadhan, Mtayarishaji KGT wa G Records, Ude Ude na Dully Sykes.
WASIFU:
JINA HALISI:Mwajuma Abdul Juma
JINA LA UTANI: Queen Darleen
KUZALIWA :Novemba 4, 1985
ALIPOZALIWA:Dar es Salaam
KAZI:Msanii

Comments