NEWCASTLE YAINYUKA LIVERPOOL

Cisse
MABAO mawili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal, Papiss Demba Cisse yalitosha kuipa Newcastle ushindi wa 2-0 dhidi ya Liverpool jioni hii, ambayo ilimaliza na wachezaji 10, hivyo kuzidi kujiimarisha katika kuwania kwake nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Msenegali aliyejiunga na Newcastle Januari mwaka huu akitokea Freiburg ya Ujerumani, sasa ametimiza mabao saba katika mechi saba alizocheza kwa mabao yake hayo ya dakika za 19 na 59 kwenye Uwanja wa St. James’ Park.
Ushindi wa Newcastle unawafanya walingane kwa pointi na Chelsea inayoshika nafasi ya tano na kupunguza idadi ya pointi wanazozidiwa na Arsenal inayoshika nafasi ya tatu hadi kubaki tano zikiwa zimebaki mechi saba za kumalizia msimu.
Katika mchezo huo, Liverpool ilimpoteza kipa wake Jose Reina dakika za mwishoni aliyelimwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Newcastle, James Perch.
Kipa huyo wa kimataifa wa Hispania, sasa atakosa mechi tatu ikiwemo Nusu Fainali ya Kombe la FA dhidi ya wapinzani wao wa Merseyside, Everton kwenye Uwanja wa Wembley, Aprili 14.

Comments