MZEE YUSUF AMPONGEZA ISHA MASHAUZI


MWANAMUZIKI  nyota wa miondoko ya taarab nchini, Mzee Yusuf ‘Mfalme’, amempongeza mkurugenzi wa kundi la taarab la Mashauzi Classic, Isha Ramadhani kwa kutwaa Tuzo ya Wimbo Bora wa Taarab katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Muziki za Kilimanjaro zilizofanyika hivi karibuni.
Mzee ambaye ni mmiliki wa kundi la Jahazi Modern Taarab, alitoa pongezi hizo Dar es Salaam jana, alipohojiwa kwa njia ya simu na mtangazaji wa Radio Times ya jijini hapa Khadija Shaibu maarufu kama Dida wa G kwenye kipindi cha Mitikisiko ya Pwani.
“Nampongeza amefanya vizuri namtakia kila la kheri... mimi nimekosa tuzo, lakini haina maana basi wengine wasipate laa, aliyepata ni vizuri kumpongeza amefanya vizuri na siku nyingine afanye vizuri zaidi.
“…Mimi nimekosa haina maana kwamba si bora, ila mashabiki wameamua hivyo nasi siku nyingine tutafanya vizuri zaidi, ninampongeza Isha na wote waliopata tuzo hizo,” alisema Mfalme.
Isha ameibuka kidedea mwishoni mwa wiki baada ya wimbo wake wa ‘Nani kama mama’ uliokuwa ukichuana na Full Stop wa mkongwe wa taarab nchini Khadija Kopa nyingine mbili za Nilijua Mtasema na Hakuna Mkamilifu za kundi la Jahazi, kuibuka mshindi wa kinyang’anyiro hicho.
Kwa upande wake, Isha ‘Jike la Simba’ alisema: “Nimejisikia poa sana ninayo furaha mpaka nahisi kutokwa na machozi... nawashuru mashabiki wangu kwa kunichagua tangu 2010 nimeingia kwenye tuzo hizo lakini sasa mashabiki wamenikubali na kuipenda kazi yangu wameamua kunisapoti kupitia njia hii.” Pia alitoa shukrani za dhati kwa mama yake Rukia Ramadhani ambaye ni mwimbaji wa taarab kwenye kundi la Tanzania One Thetre (TOT).

Comments