MSICHANA ANYWA SUMU YA PANYA SABABU YA KIFO CHA KANUMBA


MSICHANA mmoja aliyetambulika kwa jina la Mariam Elias, mkazi wa Misugusugu wilayani Kibaha, mkoani hapa, amenusurika kupoteza maisha yake baada ya kunywa sumu ya panya, kutokana na kifo cha msanii mahiri wa filamu hapa nchini, Stephen Kanumba.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini Kibaha jana, Ofisa Habari wa Shirika la Elimu Kibaha, Rose Mtei, alisema kwamba, msichana huyo alifikishwa katika hospitali Teule ya Tumbi jana usiku, majira ya saa 5:30, akiwa na hali mbaya kutokana na sumu aliyokunywa.
Mtei alisema kwamba, msichana huyo wakati alipofikishwa hospitalini hapo, hali yake ilikuwa ni mbaya, lakini madaktari waliyokuwa zamu, waliweza kujitahidi kwa hali na mali kumuhudumia kwa lengo la kuokoa maisha yake.
“Ni kweli katika hospitali yetu ya Tumbi, usiku wa tarehe 10 majira ya saa 5:30, tuliweza kumpokea msichana huyo ambaye alikuwa amekunywa sumu ya panya na alipoulizwa, alisema ni kutokana na kifo cha nguli wa tasnia ya filamu hapa nchini, Stephen kanumba,” alifafanua Mtei.
Aidha, Mtei alisema kwamba, inasemekana msichana huyo alikuwa akimpenda sana marehemu Kanumba kutokana na umahiri wake katika kuigiza filamu mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Ofisa huyo aliongeza kuwa, kwa sasa msichana huyo baada ya kupatiwa matibabu na madaktari, anaendelea vizuri na kwamba, bado yupo katika uangalizi kwa ajili ya kumfanyia uchunguzi zaidi.
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita nyumbani kwake Sinza Vatican kutokana na ugomvi wa kimapenzi, kifo kilichowagusa maelfu ya mashabiki na wadau wa filamu wa rika mbalimbali.