MAMA WA KANUMBA CHINI YA UANGALIZI WA DAKTARI


Kanumba
MAMA wa marehemu Steven Kanumba, ameanza kusumbuliwa na presha kiasi cha kulazimika kuwa chini ya uangalizi wa daktari.
Dk. Nassor Matuzya kutoka hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam ambaye amewahi kuwa Dakatri wa klabu ya Yanga, enzi za kocha Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic ameiambia bongostaz joni hii kwamba yupo kwa ajili ya kufuatilia hali ya Mama Kanumba.
“Mama anasumbuliwa na presha, inapanda sana, lakini namtibu na kwa sasa anaendelea vizuri,”alisema Dk. Matuzya.
Matuzya alisema Mama Kanumba leo usiku atapelekwa hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam kuuona mwili wa mwanawe kabla ya kuagwa na mazishi kesho.
Mama huyo aliyewasili jana kutokea Bukoba, ameridhia mwanawe azikwe Dar es Salaam, ingawa baba wa msanii huyo alipenda kijana wake azikwe karibu na kaburi la babu yake, Mzee Kanumba huko Shinyanga.
Wakati huo huo: Mwanamitindo Millenne Happiness Magesse ameongezwa kwenye kamati ya Mazishi. Millene ameonekana tangu jana akiwajibika ipasavyo kwenye msiba huo.
Kanumba ataagwa kesho kuanzia saa nne asubuhi, viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam na kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni.
Wakati huo huo: Watu wameendelea kumiminika nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican kutoa rambirambi na miongoni mwao ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Imani Omar Madega.
Madega alifika kutoa salamu zake za rambirambi na ubani kisha kuungana na waombolezaji wengine. Mwanamuziki mkongwe, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ naye alifika.  

Comments

  1. Every thing i hear about Kanumba is so sad and touching. Pole mama, Mungu atakupa nguvu, najua ni ngumu, lakini ni Mungu tu atakuwezesha, muombee mwanao, alale kwa amani.
    poleni wote. Kanumba tulimpenda wote.

    ReplyDelete

Post a Comment