KASEJA:KUTOKATA TAMAA NDIYO SIRI YA MAFANIKIO


NAHODHA wa Simba, Juma Kaseja, amesema kutokata tamaa miongoni mwa wachezaji ndiyo siri kubwa ya ushindi ambao Simba imeupata katika mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF), dhidi ya ES Setif ya Algeria.
Simba ilifunga bao katika dakika ya 90 ya mchezo wakati tayari ikiwa imefungwa mabao 3-0 na ikiwa inacheza ikiwa pungufu kwa takribani dakika 78 za pambano hilo.
Akizungumza na tovuti ya Simba, Kaseja alisema kama wachezaji wasingeamini kwamba wanaweza kupata kitu kwenye pambano lile wasingeweza kupata chochote.
"Tulikuwa katika uwanja wa ugenini. Hali ya hewa ilikuwa tofauti kabisa na ile tuliyozoea kwetu na tulikuwa pungufu kwa mchezaji mmoja muhimu. Katika hali ya kawaida, timu nyingine ingeweza kukata tamaa lakini sisi tulipiga moyo konde na tukaendelea,"alisema.
Katika pambano hilo, Kaseja alikuwa katika kiwango cha juu na kama si uhodari wake, Simba ingeweza kufungwa mabao mengi zaidi.
Kama Emmanuel Okwi asingefunga goli katika dakika ya 90 ya mchezo huo, nyota wa Simba kwa pambano hilo angekuwa Kaseja.
Hata hivyo, nahodha huyo amekataa kuchukua sifa binafsi kwa pambano hilo na kusema kiujumla kila mchezaji alitekeleza wajibu wake na ndiyo maana Simba imefuzu kwenda hatua nyingine ya Kombe la Shirikisho.
Chanzo:www.Simba.co.tz

Comments