KAMBI TWIGA STARS YAVUNJWA


TIMU ya taifa ya wanawake ya soka Tanzania, ‘Twiga Stars’ imevunja kambi yao rasmi jana hadi Aprili 22 mwaka huu watakapokutana tena.
Kambi hiyo iliyokuwa Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ruvu, ilianza Machi 25, ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya mechi ya mchujo kuwania kufuzu Fainali za Wanawake Afrika (AWC), zitakazofanyika Equatorial Guinea, Novemba mwaka huu.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka mkoani Pwani, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa, alisema kambi hiyo ilikuwa ni ya muda ili kuona uwezo wa nyota wapya aliowaita katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza.
“Tumevunja kambi leo mpaka Aprili 22 ndipo tutaendelea na kambi tena, kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo na kambi hii ya muda tulikuwa tunawapa mazoezi kidogo vijana na tumeona uwezo wao kwa kuwa ni wapya,” alisema Mkwasa.
Mkwasa alisema, katika ufundishaji wa timu hiyo, tatizo kubwa linalomkabili ni wachezaji wanaporejea makwao, akiwaita tena kambini, humpa wakati mgumu wa kuanza upya kile ambacho alikifundisha toka awali.
Twiga Stars katika kibarua hicho cha kufuzu, itavaana na Ethiopia ugenini Addis Ababa Mei 26 mwaka huu, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.

Comments