KAMATI YA TIBAIGANA HAIKUJADILI POINTI ILIZOPOKONYWA YANGA

Tibaigana
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesikitishwa na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo namba 132 wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yao na Azam uliofanyika Machi 10 mwaka huu.
Vilevile imesikitishwa na uongozi wa klabu ya Yanga kushindwa kuvikemea hadharani vitendo hivyo vilivyofanywa na wachezaji wake.
Kamati hiyo ilikutana jana (Aprili 4 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana kujadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Yanga kupinga uamuzi uliofanywa na Kamati ya Ligi ya TFF dhidi ya wachezaji hao.
Mbele ya Kamati hiyo, Yanga ilikuwa na rufani mbili. Rufani ya kwanza ya Machi 11 mwaka huu iliomba matokeo ya mchezo huo yafutwe, ikiwemo kadi walizooneshwa wachezaji wao na mwamuzi aadhibiwe kwa kushindwa kumudu mchezo huo.
Wakati ikifanya mawasilisho (submissions) mbele ya Kamati, Yanga iliamua kuondoa rufani hiyo kwa vile katika ya pili iliyokatwa Machi 14 mwaka huu ikipinga adhabu zilizotolewa ina kifungu (j) kilichodai Kamati ya Ligi ya TFF ilikosea kutotoa uamuzi wowote kwa refa aliyedaiwa kutoa maneno ya kashfa na kejeli kwa wachezaji wao.
Baada ya kusikiliza submissions za pande zote mbili (walalamikaji- Yanga) ambao walikiri hatia ya vitendo hivyo na kuomba wachezaji wake wapunguziwe adhabu, na (walalamikiwa- TFF), Kamati imetoa uamuzi ufuatao;
Mchezaji Nurdin Bakari amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu za ligi na faini ya sh. milioni moja. Omega Seme amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu na faini ya sh. milioni moja.
Nadir Haroub atatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ambayo haikatiwi rufani. Lakini Kamati ya Nidhamu imeondoa adhabu ya mechi nyingine tatu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa vile hizo atazitumikia kwa pamoja, lakini adhabu ya faini ya sh. 500,000 inabaki, hivyo atalipa jumla ya sh. milioni moja.
Stephano Mwasika ambaye alifungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja, adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za msimu wa ligi 2011/2012, lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili.
Kwa upande wa Jerryson Tegete aliyefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000, adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za ligi msimu huu (2011/2012), lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili.
Adhabu ya Yanga kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake inabaki kama ilivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1). Vilevile adhabu ya faini ya sh. 500,000 kutokana na timu hiyo kupata kadi tano na kuendelea kwenye mechi moja inabaki kama ilivyo vile kanuni ya 25(1) haikatiwi rufani.
Kamati imesema adhabu zimeanza kutumika tangu zilipotolewa na Kamati ya Ligi, hivyo kwa ambapo tayari wameshatumikia mechi kadhaa zinahesabika. Kwa watakaoshindwa kulipa faini wataendelea kuwa nje ya uwanja mpaka fedha hizo zitakapolipwa.
Mwenyekiti Tibaigana amewataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji wao, na makosa hayo yakijirudia adhabu kali zaidi zitatolewa.
Pia Kamati ya Nidhamu ya TFF haikujadili suala la Yanga kunyang’anywa pointi tatu katika mchezo kati yake na Coastal Union kwa vile hakukuwa na rufani hiyo mbele yake.
TFF YALAANI MAUAJI YA BOSI WA FA SOMALIA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amepokea kwa masikitiko taarifa za shambulizi la kigaidi lililofanywa jana asubuhi (Aprili 4 mwaka huu) jijini Mogadishu, Somalia na kupoteza maisha ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Somalia (SFF), Said Mohamed Nur.
Kwa niaba ya TFF na wadau wa mpira wa miguu Tanzania anatuma salamu za rambirambi kwa Makamu Mwenyekiti wa SFF, Ali Said Ghuled kutokana na kifo hicho cha ghafla cha shambulizi la bomu cha Nur ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Amesema Nur alishiriki kikamilifu katika kujenga maisha ya wananchi wa Somalia kwa kupitia mpira wa miguu, hivyo analaani kwa nguvu vitendo vya kigaidi ambavyo pia vimepoteza maisha ya watu wengine katika tukio hilo.
Kwa kipindi chote cha maisha yake, Nur ameutumikia mpira wa miguu katika ngazi tofauti nchini kwake na ukanda huu wa CECAFA, hivyo kifo chake ni pigo kwa Tanzania, na daima itaendelea kukumbuka mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu.
Rais Tenga amesema TFF iko pamoja na familia ya Marehemu katika kuomboleza msiba huu mzito na kuwataka wawe na uvumilivu na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa kwao.
Kwa mechi zote za TFF zitakazochezwa katika kipindi cha siku 7 zijazo kutakuwa na dakika moja ya kusimama kimya kwa ajili ya kuomboleza msiba huo. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amina.
KILA LA KHERI SIMBA ALGERIA
Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Simba kesho (Aprili 6 mwaka huu) wanapambana na ES Setif katika mchezo wa marudiano wa kombe hilo.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaitakiwa kila la kheri Simba kwenye mechi hiyo kwani ina uwezo wa kupata matokeo mazuri yatakayoivusha katika raundi inayofuata. Msafara wa Simba unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Dk. Sylvester Faya.
Mechi hiyo namba 46 itachezeshwa na waamuzi Ben Hassan Mohamed, Hmila Anouar, Ben Abdelmoumen Kamel na Kordi Med Said, wote kutoka Tunisia. Kamishna atakuwa Jean Fidele Diramba kutoka Gabon.
Powered by Sorecson : Creation de site internet
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments