JUMA NYOSO ALIZWA NA KADI NYEKUNDU YA ES SETIF

HAKUNA mtu aliyekuwa na furaha baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa katika pambano baina ya Simba na ES Setif ya Algeria kama Juma Nyoso.
Nyoso alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 12 tu ya mchezo baina ya timu hizo mbili na kama Simba ingetolewa kwenye michuano hiyo, huenda lawama nyingi zingeelekezwa upande wake.
Akielezea namna tukio hilo lilivyokuwa, Nyoso alisema mshambuliaji wa Setif, Akram Djanit, alikuwa akimvuta jezi bila sababu kila wakati na wakati yeye naye alipomsukuma ili asimghasi, mchezaji huyo alianguka chini kama ameangukiwa na tofali.
"Yule jamaa inaonekana alikuwa anatafuta mtu wa kumsababishia kadi tu. Tangu mpira umeanza yeye alikuwa akituchokoza na kututukana muda wote. Mara akuvute jezi, mara akutwange kichwa na ukimgusa tu kwenye eneo la hatari anajiangusha kutafuta penalti. Huo ndiyo ulikuwa mchezo wake," alisema.
Mara baada ya mapumziko, Nyoso alikutwa na wachezaji wenzake akiwa analia katika chumba cha kubadilishia nguo na ameieleza tovuti ya Simba kwamba alilia kwa sababu alijua amewaangusha wenzake.
"Unajua kabla ya mechi tulizungumza kwa kirefu sana na wenzangu kuhusu mbinu za Waarabu wanapokuwa kwao. Tulikuwa tumejiandaa vema kisaikolojia lakini ndiyo hivyo kwenye mchezo kuna wakati unajisahau na ndicho kilichonikuta," alisema.
Nyoso ambaye ni nahodha msaidizi wa Simba amewashukuru wachezaji wenzake kwa kuiwezesha Simba kufuzu hata kama ilifungwa kwa vile imesababisha bendera ya Tanzania kuzidi kupeperushwa barani Afrika.
Chanzo:www.Simba.co.tz

Comments