HATIMAYE AZIM DEWJI AWAJAZA MANOTI WACHEZAJI WA SIMBA SC



HATIMAYE mdau mkubwa wa klabu ya soka ya Simba Azim Dewji leo amekabidhi kitita cha shilingi milioni 15 kwa wachezaji wa klabu hiyo kama zawadi ya kutinga 16 bora ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF). 
Dewji amekabidhi fedha hizo baada ya mtandao huu jana  kuripoti taarifa za mfadhili huyo wa zamani wa Simba kupiga chenga kutimiza ahadi hiyo aliyoitoa wiki iliyopita baada ya Simba kutinga hatua hiyo kwa kuiondoa Es Setif ya Algeria. 
Habari kutoka katika kambi ya klabu ya Simba iliyopo Bamba Beach Kigamboni jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa Dewji alitinga kambini hapo asubuhi ya leo na kukabidhi fedha hizo kwa viongozi wa benchi la ufundi la Simba.
 Taarifa zinaeleza kuwa Dewji aliwaeleza wachezaji hao kuwa alishindwa kutoa fedha hizo kwa wakati aliopanga kutokana na kusubiri kuanza kwa kambi ambapo aliamini wachezaji wangekuwepo wote. 
“Tunashukuru bwana Dewji hatimaye amepeleka zile fedha alizokuwa akizitangaza kwenye vyombo vya habari kuwa atawapa wachezaji kutokana na kusonga mbele kwenye kombe la CAF,”Aliongeza kiongozi huyo. 
Katika hatua nyingine, kikosi cha wachezaji wa timu hicho kilichopo kambini kinaendelea na maandalizi yake ya michezo yake ya ligi kuu soka Tanzania Bara na ule wa Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan Aprili 22 kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaa. 
Simba inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 50 keshokutwa itashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Saalam kukwaana na maafande wa Ruvu Shooting.




Comments