HATA MTIBWA IKISHUSHWA DARAJA, SIMBA BINGWA TU NA YANGA MAUMIVU PALE PALE




Simba SC, mabingwa watarajiwa

MEI 5, mwaka huu nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitawaka moto kwa mpambano mkali wa watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ingawa mchezo huo unachukuliwa kama wa kukamilisha ratiba tu, kwa kuwa Simba ilikwishajisogeza jirani na ubingwa na Yanga imekwishatoka kwenye matumaini ya kupata hata nafasi ya pili, baadhi wana dhana tofauti- tena inayowadanganya.
Hiyo inafuatia kuvunjika kwa mechi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Azam, Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam wiki iliyopita, wanadhani mambo yamebadilika.
Mtibwa ndiyo walikuwa sababu ya kuvunjika mechi hiyo, baada ya kugomea penalti, na matokeo yake Kamati ya Ligi Kuu imewapa ushindi Azam.
Lakini katika kutoa adhabu, Kamati ya Ligi Kuu imeonyesha mapungufu kulingana na kanuni inavyosema; kwamba timu inayosababisha mechi kuvunjika inashushwa daraja. Wao hawajatoa adhabu kwa ukamilifu kulingana na maelekezo ya kanuni.
Nini kinachofuata Mtibwa ikishushwa daraja? Matokeo yake yatafutwa, ina maana timu zilizonufaika kwa kubeba pointi nyingi dhidi ya Mtibwa, yenye maskani yake Uwanja wa Manungu, Turiani ambayo tangu ipande Ligi Kuu mwaka 1996, haijawahi kushuka zitaathirika.
Simba ni timu pekee iliyovuna pointi zote sita kwa Mtibwa, kwanza ikiifunga 1-0 Septemba 25, mwaka jana mjini Morogoro na baadaye 2-1 katika mchezo wa marudiano Machi 18, mwaka huu.
Azam ilivuna pointi tatu tena za mezani, kwani mechi ya kwanza Oktoba 25, mwaka ilifungwa 1-0 kabla ya mechi ya marudiano iliyovunjika na Yanga ilivuna pointi nne, kutokana sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza Septemba 11, mwaka jana kabla ya kushinda 3-1 katika mchezo wa marudiano Februari 8, mwaka huu.
Iwapo adhabu ya Mtibwa ingetokana na maelekezo ya kanuni, Azam ingenufaika zaidi- kwa sababu ingekatwa pointi tatu, wakati Simba ingekatwa pointi sita na Yanga pointi nne.
Kwa sasa Simba ina pointi 59 na ikishinda mechi ya mwisho itatawazwa rasmi kuwa bingwa, kwa kufikisha pointi 62, lakini kama Mtibwa itashushwa daraja, Wekundu wa Msimbazi watamaliza na pointi hizo hizo 59 iwapo wakiifunga Yanga katika mechi ya mwisho.
Azam wana pointi 51 na wakishinda mechi zao mbili za mwisho dhidi ya Polisi na Toto, watafikisha pointi 57- lakini Mtibwa ikishushwa watamaliza na pointi 54. Ina maana hata kama Simba ikifungwa na Yanga na Mtibwa ikashushwa, bado Azam hawawezi kuwa mabingwa- wazipate wapi pointi 56? Baadaye sana!
Kama Mtibwa ikishushwa, katika hesabu zake za sasa Yanga itajiongezea pointi moja tu, je wataipiku Azam? Jua la mwakani.
Nataka niwaambie tu wadau wenye kudhani Mtibwa ikishushwa Top 3 ya Ligi Kuu ya Bara itabadilika, wanajidanganya. Itabaki vile vile.

MECHI ZA MTIBWA DHIDI
YA TOP 3 LIGI KUU BARA
J’tano 07/09/11  Mtibwa    0 – 0    Yanga
J’nnee 25/10/11 Mtibwa    1 – 0   Azam
J’pili   25/09/11  Simba      1 – 0   Mtibwa Sugar
J’tano 08/02/12  Yanga      3 – 1   Mtibwa Sugar
J’pili   18/03/12  Simba      2 – 1   Mtibwa Sugar
J’tatu  23/04/12  Azam       1 – 1   Mtibwa Sugar 
(Mechi ilivunjika, Azam ikapewa pointi tatu)
CHANZO:BONGOSTAZ

Comments

  1. Simba inapoint 59 sasa Mtibwa ikishushwa atakuwa na point 53 na wakishinda mpambano wa mwisho dhidi ya Yanga watakuwa na 56.
    Wakati Azam wanapoint 53 (+point 3 za mezani) Mtibwa wakishushwa wanakuwa na point 50. Wakiifunga Kagera na Toto wanafikisha point 56.

    ReplyDelete

Post a Comment