Skip to main content

HALI SI SHWARI YANGA, NCHUNGA AITISHA KIKAO CHA DHARURA


SIKU chache baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kuanza kumeguka, mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga ameitisha kikao cha dharura.
Hivi karibuni wajumbe wawili wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Sarah Ramadhan na Seif Ahmed pamoja na mjumbe wa usajili Abdallah Binkleb walitangaza kujiuzuru nyadhifa zao kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wa viongozi wa juu.
Habari za uhakikika zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinaeleza kuwa kikao hicho kitakachohusisha viongozi wa kamati ya utendaji kinatarajiwa kufanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mmoja ya viongozi wa Yanga aliliambia gazeti hili kwamba Nchunga amelazimika kuitisha kikao hicho cha dharura ili kujadili mustakabali mzima wa hali ya sintofahamu inayoendelea ndani ya klabu hiyo.
Kiongozi huyo alisema pamoja na hali hiyo, kikao hicho pia kitajadili mwenendo mzi,ma wa timu hiyo ambayo tayari imeshapoteza ndoto za kutetea ubingwa wake baada ya kufanya vibaya katika michezo yake kadhaa.
“Ni kweli Mwenyekiti wetu ameitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji hiyo kesho (leo) kubwa zaidi ni hali tete inayoendelea ndani ya klabu yetu,”Alisema.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Nchunga kwa simu yake ya kiganjani simu yake iliita bila ya kupokelewa.
Hivi karibuni baadhi ya wanachama wakiongozwa na mwenyekiti wa matawi ya Yanga Mohammed Msumi waliutaka uongozi wote wa Yanga ujiuzulu baada ya kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo katika msimu huu kama walivyoahidi wakati wakiomba kura.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Yanga waliwataka Wanayanga kutulia kwanza na kuwapa nafasi viongozi kufanya tathmini kwanza, huku Nchunga ambaye alikuwa nje ya nchi kikazi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa hatojiuzulu.
Tangu kuingia madarakani kwa Nchunga ambaye chini ya uongozi wake waliweza kutwaa mataji matatu, mbali na hali iliyotokea hivi karibuni, kulikuwepo na msigano baina yake na Makamu wake Mwenyekiti Davis Mosha ambaye aliamua kujiuzulu nafasi yake hiyo.

Comments