DIAMOND ANG'ARA TUZO ZA KILI 2012


Diamond akipongezwa
Khadija kopa
Roma katikati, kulia Profesa Jay na kushoto said Fela
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe akimpa tuzo Diamond

MSANII Nassib Abdul ‘Diamond’ usiku huu ameng’ara kwenye tuzo za Kilimanjaro Music Award, baada ya kujinyakulia tuzo tatu.
“Namshukuru Mungu, wakati mwingine uvumilivu na subira ni mzuri. Mwaka jana sikupata tuzo, nikamshukuru Mungu, nikaongeza bidii, nikafanya kazi nzuri, leo ninachukua tuzo ya tatu sasa hivi, alisema Diamond kuambia bongostaz baada ya kushinda tuzo ya Video Bora ya Mwaka, kupitia wimbo Moyo Wangu, ambayo ilikuwa ya tatu usiku huu.
Diamond alizishinda nyimbo za Hakunaga ya Suma Lee, Wangu ya Jay Dee, Ndoa Ndoana ya Kassim na Bongo Fleva ya Dully Sykes.
Barnaba aliibuka Mwimbaji Bora wa Kiume, akiwashinda, Ally Kiba, Diamond, Belle 9 na Mzee Yussuph.
Tuzo ya waliochangia mafanikio ya muda mrefu ilikwenda kwa JKT Taarab, marehemu Dk Remmy Ongala na King Kiki.
Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ alishinda tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike, akiwashinda Linah, Khadija Kopa, Dayna na Isha Mashauzi.
Ommy Dimpoz aliwabwaga Darasa, Rachel, Abdul Kiba na Beatrice aka Nabisha katika tuzo ya Msanii Anayechipukia.
Ommy Dimpoz alimpa nafasi Diamond kuelezea namna prodyuza mmoja alivyomkatisha tamaa wakati anaanza muziki.
“Nilimpeleka Ommy kwa prodyuza wangu, nikamuambia msaidie huyu kijana, anaweza naye ainuke kama sisi, lakini yule prodyuza akasema dogo hawezi kuimba. Ila wimbo ule ule, amerekodi na leo unampa tuzo,”alisema Diamond.
Katika wimbo bora wa mwaka, mshindi alikuwa ni Suma Lee kupitia wimbo wake Hakunaga, akiwashinda Ally Kiba na Dushelele, Diamond na Moyo Wangu, Roma na Mathematics, Nilipe Nisepe wa Belle 9 na Riz One wa Izzo B.
Bahati mbaya Suma Lee hakuwepo na tuzo zake alichukuliwa na Babu Tale.
Katika wimbo bora wa Zouk Rhumba, Ally Kiba, kupitia wimbo wake Dushelele aliwabwaga Barnaba na wimbo wake Daima Milele, Dayna na Nivute Kwako Lady Jaydee, aliyemshirikisha Mr Blue katika Wangu na Kizunguzungu wa Rachel.
Diamond alibeba tuzo ya Mtunzi  Bora wa Mwaka, akiwaangusha Ally Kiba, Mzee Yussuph, Barnaba na Belle 9, wakati wimbo bora wa kushirikiana, Ommy Dimpoz na Ally Kiba waling’ara kupitia kibao chao Nai Nai, Famous wa Jay Mo na P Funk, King Zilla wa Godzilla na Marco Chali na Wangu wa Jay Dee na Mr. Blue na Kama ni Gangstar wa Chege, Mh Temba na Ferooz.
Katika wimno bora wa Raggae, kibao cha Arusha Gold cha Warriors From East kiling’ara mbele ya Mazingira wa Malfred aliyemshirikisha Lutan Fyah, Give It Up To Me wa Delyla Princess, Nia Yao wa  20% na Ni Wewe wa Nakaaya.
Katika wimbo bora wa Ragga, Dancehall, Maneno Maneno wa Queen Darleen, ulizishinda Good Look wa AY aliyemshirikisha Miss Trinity, Ganja Man wa Dabo, Kudadeki na Poyoyo za Malfred.
Katika wimbo bora wa Taarab, Isha Mashauzi kupitia wimbo wake Nani Kama Mama uliushinda wimbo wake Mama Mashauzi, Full Stop wa Khadija Kopa, Hakuna Mkamilifu na Nilijua Mtasema za Jahazi.
Katika wimbo bora wa Kiswahili wa bendi, African Stars ‘Twanga Pepeta’ liling’ara kupitia wimbo wa Dunia Daraja ikizishinda Mashujaa na
Hukumu ya Mnafiki na Mtenda za Extra Bongo na Falsafa ya Mapenzi, Mapacha Watatu na Usia wa Babu.
Rapa bora wa bendi wa mwaka alikuwa ni Kalidjo Kitokololo wa FM Academia, aliyewashinda Khalid Chokoraa, Feguson, Msafiri Diouf na Totoo ze Bingwa.
Msafiri Diouf alipanda jukwaani na kukiri kushindwa- akimwagia sifa Kitokololo kwamba alistahili.
Katika wimbo bora wa Afri Pop, Suma Lee aliibuka mshindi kutokana na kibao chake Hakunaga, kilichozishinda Bongo Fleva wa Dully Sykes, Moyo Wangu na Mawazo za Diamond na Nai Nai wa Ommy Dimpoz.
Katika Mtumbuizaji Bora wa Kiume, Diamond aliwaangusha Ally Kiba, Dully Sykes, Bob Junior na Mzee Yusuph, wakati Mtumbuizaji Bora wa Kike, Khadija Kopa aliwaangusha Isha Mashauzi, Queen Darleen, Dayna na Shaa.
Katika wimbo bora wa R&B, Ben Pol kupitia kibao chake My Number Fun, kiliushinda wimbo wake Maumivu, Nilipe Nisepe wa Belle 9, Usiniache wa Hemed na Napata Raha wa Jux.
Roma aliibuka kidedea katika wimbo bora wa Hip hop, kupitia wimbo wake Mathematics, uliozishinda Famous, King Zilla, Riz One na Kilimanjaro.
Roma aling’ara pia katika tuzo ya Msanii Bora wa Hip Hop, akiwashinda Godzilla, Izzo B, Joh Makini na Fid Q.
Baada ya kuchukua tuzo hiyo pia, Roma aliwaambia wasanii wengine wa Hip hop kwamba anastahili.
Jaguar wa Kenya alishinda tuzo ya wimbo bora wa Afrika Mashariki, kupitia wimbo wake Kigeugeu, uliozishinda Chokoza, Mulika Mwizi, Coming Home na 4 Sho 4 Shizzle.
Maneka wa AM Records alishinda tuzo ya Mtayarishaji Bora wa Nyimbo, akiwaangusha Marco Chali, Pancho Latino, Bob Junior na Man Walter.

BURUDANI ILIPOOZA:
Sambamba na utoaji wa tuzo, kulikuwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali- lakini kwa ujumla sekta hiyo mwaka huu ilidorora.
Si kwa sababu ya wasanii wa Tanzania pekee kutumbuiza, la hasha- bali watumbuizaji wenyewe walishindwa kusisimua watu.
Angalau kidogo Khadija Kopa aliwarusha watu, lakini wengine walipitisha ratiba tu.

Comments

Post a Comment