CRDB BANK, PRIME TIME ZACHUANA TENDA YA TIKETI TFF

Kampuni nne kati ya sita zimepita hatua ya kwanza ya mchakato wa kupata moja itakayofanya kazi ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na nyingine zinazosimamiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Shughuli ya ufunguzi wa maombi ya hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ilifanywa jana (Aprili 19 mwaka huu) na Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho.
Kampuni ambazo zimepita hatua hiyo ya kwanza sasa zinatakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao kwa ajili ya shughuli hiyo ndani ya kipindi cha wiki tatu tangu ulipofanyika ufunguzi wa hatua ya kwanza.
Baadaye Bodi ya Tenda itakutana tena kupitia tenda zitakazokuwa zimewasilishwa na kufanya uteuzi wa kampuni moja itakayofanya kazi hiyo.
Kampuni ambazo zimefanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya pili ni CRDB Bank PLC, SKIDATA People Access Inc., Prime Time Promotions na Punchlines (T) Limited.

Comments