CANNAVARO AIPOKONYA YANGA POINTI TATU

KAMATI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania katika kikao chake cha leo jioni imeipokonya klabu ya Yanga pointi tatu kufuatia rufaa ya Coastal Union ya Tanga, dhidi ya beki Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’.
Coastal ilikata rufaa baada ya kufungwa 1-0 na Yanga Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikipinga klabu hiyo kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye inadai alikuwa hajamaliza adhabu yake ya kukosa mechi tatu baada ya kupewa kadi nyekundu kwa vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam FC
Akizungumza na bongostaz dakika chache zilizopita, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wallace Karia alisema maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao ambacho yeye hakuhudhuria.
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti), ambaye hakuhudhuria Damas Ndumbaro, Steven Mnguto, Geoffrey Nyange, Seif Ahmed, Henry Kabera, ACP Ahmed Msangi, Meja Charles Mbuge na Ahmed Yahya.
Hata hivyo, Yanga iliamua kumtumia Cannavaro baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, Alfred Tibaigana kusitisha adhabu zote zilizotolewa na Kamati ya Ligi kuwafungia wachezaji watano wa Yanga kwa kufanya fujo kwenye mechi na Azam FC, ikiwemo kumpiga refa.
Tibaigana alisitisha adhabu zote akidai kwamba Kamati ya Ligi haina mamlaka ya kutoa adhabu, ispokuwa Kamati yake.
Kamati ya Tibaigana ilipanga kukutana kesho Jumanne kujadili suala hilo, baada ya kusitisha adhabu hiyo kwa wiki mbili. 

Comments