BANGO LA TFF LEO

WAGANDA KUCHEZESHA NGORONGORO VS SUDAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Uganda kuchezesha mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan itakayofanyika Aprili 21 mwaka huu.
Mwamuzi atakayechezesha mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni ni Brian Miiro. Waamuzi wasaidizi ni Mark Ssonko na Lee Patabali wakati mwamuzi wa mezani ni Denis Batte.
Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15. Kamishna na waamuzi hao watawasili nchini Aprili 19 mwaka huu kwa ndege za Ethiopian Airlines na Air Uganda.
KINYANG’ANYIRO VPL KUENDELEA APRILI 18
Kinyang’anyiro cha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kinaendelea tena kesho (Aprili 18 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa kwenye miji ya Bukoba, Mwanza, Dar es Salaam, Mlandizi na Dodoma.
Mabingwa watetezi Yanga watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba wakati Toto Africans itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Vinara wa ligi hiyo Simba wataoneshana kazi na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Ruvu Shooting na Moro United zitaumana kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Nayo Polisi Dodoma itakuwa mwenyeji wa Coastal Union mjini Dodoma.
TENDA YA TIKETI KUFUNGULIWA APRILI 18
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 18 mwaka huu) itafungua maombi ya tenda zilizowasilishwa na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza tiketi za elektroniki.
Maombi hayo yatafunguliwa saa 9 alasiri kwenye ofisi za TFF ambapo kampuni zote zilizowasilisha tenda zinatakiwa kuwepo wakati wa ufunguzi huo.
Machi 9 mwaka huu TFF ilitangaza tenda kwa ajili ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na mechi nyingine azozisimamia.

Comments