BABA MZAZI WA KANUMBA ASEMA MALARIA ILIMFANYA ASIHUDHURIE MAZISHI YA MWANAE


Kutoka blogu ya bongostaz tunaelezwa kuwa BARUA iliyotumwa na wawakilishi watatu wa baba wa marehemu Steven Kanumba, Chales Kanumba, imesomwa jana mbele ya vyombo vya habari nyumbani kwa marehemu.
Katika barua hiyo baba huyo alieleza kuwa ameshindwa kufika kwenye msiba baada ya kuugua malaria na kuandikiwa sindano za masaa.
Barua hiyo iliyotumwa kwa kamati ya mazishi na ndugu wa familia ilisema: “Salamu katika bwana, kwanza nawashukuru kwa sana kwa kunitumia usafiri Mungu awe nanyi.”
“Napenda kuwajulisha kuwa tangu jana (Jumapili), nilikuwa na malaria vidudu 15 na kuandikiwa sindano za masaa, ilipofika saa 12 asubuhi nikaanza kutapika na kupelekwa hospitali.”
“Nilipofika hospitali nikapimwa na kukutwa na presha ya kupanda kiwango cha 180 kwa 140 (kawaida 120 kwa 80), hadi sasa naona kizunguzungu, hivyo nawatuma wawakilishi wangu watatu, Michael Kanumba, Mbanakheli Kanumba na Clisant Kanumba.”
Pamoja na barua hiyo pia mama mzazi wa marehemu na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) walitoa shukrani zao kwa wote waliyohusika kwa namana yoyote.
Mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mutegoa, alitoa shukrani zake na kuwaaga waandishi wa habari akisema anaenda kuliangalia kaburi la mwanae, ambaye alizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni.
Naye Rais wa shirikisho hilo la filamu Simon Mwakifwamba, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na viongozi wote waliyohusika.
Msanii mwingine aliyeibuliwa na marehemu Kanumba, Emanuel Myamba, aliwaomba wananchi kutulia na kuachia mahakama ifanye kazi yake bila kuingiliwa kuhusiana na kifo chake Kanumba.

Comments