AZAM WAIPINDUA YANGA LIGI KUU

Nyota wa Azam
AZAM FC imerejea katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 4-1 jioni hii kwenye Uwanja wa azam, Chamazi, Dar es Salaam.
Shukrani kwao Mrisho Khalfan Ngassa aliyefunga mabao mawili dakika za 30 na 72, John Raphael Bocco aliyefunga moja dakika ya 44 na Herman Kipre Tcheche aliyefunga lingine dakika ya 50.
Kwa matokeo hayo, Azam imefikisha pointi 47, moja zaidi dhidi ya mabingwa watetezi Yanga wenye 46. Hata hivyo, Azam na Simba inayoongoza ligi kwa pointi zake 59, zimecheza moja zaidi dhidi ya Yanga, 22-21.
Dhahiri mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ni za farasi watatu, ladha ambayo imekosekana kwa muda mrefu nchini kutokana na SImba na Yanga pekee kutawala ligi hiyo.
Timu tofauti na Simba na Yanga ya mwisho kubeba ndoo ya ubingwa wa Bara, ilikuwa ni Mtibwa Sugar ya Morogoro mwaka 2000, ilipotwaa kwa misimu miwili mfululizo taji hilo 1999 na 2000 na tangu hapo Kombe hilo limekuwa likabadilisha mitaa miwili tu, Jangwani na Msimbazi.

Comments