AZAM WAINASA SIMBA, REFA AKIONA CHA MOTO


BEKI wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Aggrey Morris Ambroce leo amekuwa shujaa wa klabu yake, Azam FC kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, baada ya kuifungia bao pekee dakika ya 83 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi Dodoma.
Ushindi huo, unaifanya Azam itimize pointi 50, sawa na Simba SC ambayo sasa inaongoza ligi hiyo kwa mabao tu zaidi ya kufunga.
Katika mchezo huo Polisi Dodoma, ilipata pigo baada ya beki wake, Bakari Omari kutolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika ya 57 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Refa  wa mchezo huo alipigwa na mashabiki kwa madai ya kuwapendelea Azam, baada ya mpambano kukamilika, lakini askari walifanikiwa kumuokoa asipokee kipondo zaidi.
Katika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro JKT Ruvu ililazimisha sare na wenyeji Mtibwa Sugar 1-1, wageni wakianza kupata bao kupitia kwa Bakari Kondo dakika ya 27 na wenyeji wakisawazisha kupitia kwa Saidi Bahamuzi kwa mkwaju wa penati.
Katika mechi nyingine, Kagera Sugar ilitoka 1-1 na African Lyon, Moro United 2-2 na JKT Oljoro. Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo kati ya Ruvu Shooting na Simba Uwanja wa Taifa,
Toto Africa na Yanga Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Villa Squad na Coastal Union Uwanja wa Azam, Chamazi .

Comments