ZITTO ATAKA STARS IVUNJWE, POULSEN ATIMULIWE


Na Khatimu Naheka
KIWANGO kilichoonyeshwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, katika mechi dhidi ya Msumbiji, kimesababisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kutamka kuwa amekerwa na kiwango hicho na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya maamuzi magumu ya kuvunja timu hiyo.
Stars inayonolewa na Jan Poulsen ambayo juzi ilivaana na Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuambulia sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2013), ilishindwa kuwafurahisha mashabiki baada ya kutoonyesha uwezo mzuri.
Akizungumza muda mfupi baada ya mechi hiyo, Zitto alisema kuwa kuna haja ya TFF kufanya maamuzi ya kukibadili kikosi hicho ambapo kwanza wanapaswa kusitisha mkataba wa Poulsen ambaye ameonekana kushindwa kusonga mbele.
Aliongeza kuwa mbali na kuondolewa kwa Poulsen, pia timu inatakiwa kuvunjwa na kuitengeneza upya kwa kutafuta vijana wadogo kwa kuwa wachezaji waliopo wameshindwa kuonyesha uwezo wa juu.
“Nimechukizwa sana leo (juzi) na kiwango kilichoonyeshwa na timu yetu, nadhani kuna jambo linahitajika kufanyika haraka na kwa kuanzia TFF waangalie ni namna gani wanaweza kumtimua huyu Poulsen, ni dhahiri ameshindwa kuibadilisha timu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Pia waivunje hii timu kwa sababu wachezaji wengi wameshindwa kubadilika hali inayowafanya kila siku kuwa na matatizo yaleyale. Kwa hali hii kila siku timu itazidi kutengeneza mashabiki wa kuichukia kuliko wa kuipenda.”

Comments