ZIMBABWE YAIMEZEA MATE TWIGA STARS

Chama cha Mpira wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) kimeomba mechi ya kirafiki kati ya timu yake ya Taifa ya wanawake na Twiga Stars. Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 28 au 29 mwaka huu jijini Harare.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya timu ya Zimbabwe kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Twiga Stars ambayo iko kambini mkoani Pwani tangu Machi 25 mwaka huu chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa nayo inajiwinda kwa fainali hizo ambapo itacheza mechi ya kwanza Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa dhidi ya Ethiopia. Zimbabwe yenyewe inacheza na Senegal.
Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ili ishiriki vyema michuano ya AWC.
Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Katika uzinduzi huo, Waziri Dk. Mukangara alichangia sh. milioni moja.

Comments