YANGA WALIANZA KUONJA FITNA YA ZAMALEK BONGO

SIKU mbili kabla ya kucheza mechi ya marudiano na Zamalek ya Misri, mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, wameanza kulia kufanyiwa mizengwe kabla hata ya kwenda huko.
Msafara wa Yanga, uliondoka jana alfajiri kwa ndege ya Shirika la Misri, kwenda Cairo, Misri, tayari kwa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kupigwa kesho kwenye uwanja wa jeshi jijini humo.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam juzi, zinaeleza kuwa mizengwe hiyo ilianza kutokea wakati wa kusaka viza za kuwawezesha kuingia nchini humo ambaPo ubalozi uliwatilia ngumu kidogo viongozi wa Yanga.
Mmoja ya viongozi wa Yanga alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa baada ya kupeleka maombi yao ya viza, ubalozi ulitoa kwa watu wanne tu, huku ukidai baadhi ya masuala kukamilishwa ili kuwapatia na wengine.
“Mimi nadhani ile ilikuwa ni mizengwe tu ya Waarabu katika kutumaliza mapema kisaikolojia, hivi inakuwaje mtu upeleke maombi ya jumla, halafu wachache wapitishwe na wengine wazuiwe wakati sifa ni zilezile?”
Kiongozi huyo aliongeza kuwa jambo hilo halikuwashtua sana kwani walishajipanga kukabiliana na hali yoyote ambayo wangekumbana kabla na baada ya kwenda Misri; kikubwa ni kuwa wamejipanga vema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na hatimaye kusonga mbele.
Msafara wa watu 40 wa klabu hiyo, ambao ndani yake kuna wachezaji 20 na viongozi watano, umeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa.
Wachezaji walioondoka jana ni pamoja na Shaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Chacha Marwa, Godfrey Taita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Omega Seme, Davies Mwape, Pius Kisambale, Oscar Joshua, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Job Ibrahim, Stefano Mwasyika, Kenneth Assamoh na  Shamte Ally.
Pia wamo kocha mkuu, Kostadin Papic, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, kocha wa makipa Mfaume Athuman, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, Katibu Mwesigwa Selestine, pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Tito Ossoro, Theonest Rutashoborwa, Seif Ahmed  na Ally Mayai Tembele.
Katika mechi ya awali iliyopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, hivyo ili Yanga iweze kusonga mbele inahitaji kushinda au sare ya mabao kuanzia mawili.

Comments