YANGA WAINGIA MAFICHONI KUKWEPA MASHABIKI

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, imejificha kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika Masaki, kujiandaa na mechi yao dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Mechi baina ya timu hizo, inatarajiwa kupigwa Machi 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga na Kocha wa Yanga, Kostadin Papic, anauchukulia mchezo huo kama fainali.
Papic, ameamua kubadili uwanja wa mazoezi kutoka ule wa Shule ya Sekondari Loyola uliopo Mabibo hadi huo wa Tanganyika bila ya kueleza sababu, ingawa inadhaniwa ni kukwepa kutizamwa na mashabiki.
Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kwamba wanashukuru hadi sasa hakuna majeruhi mpya kwenye kikosi chao, zaidi ya kipa Yaw Berko anayeuguza goti.
Aliongeza kuwa wachezaji wanajifua kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo na mingine yote iliyobaki, ili kuhakikisha wanatetea ubingwa wao.

Comments