YANGA KIBARUA KIGUMU CAIRO LEO

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, leo watakuwa na kibarua kigumu watakaposhuka Uwanja wa Jeshi jijini Cairo, Misri, kukwaana na wenyeji Zamalek ikiwa ni mechi ya marudiano raundi ya kwanza.
Yanga ambayo iliwasili Cairo tangu juzi na kufikia Hoteli ya Holiday Inn, ilikumbana na baridi kali iliyofikia nyuzi joto 16 na kuonekana kuwachosha wachezaji na viongozi, ambao hawakutarajia kukutana na hali kama hiyo.
Pamoja na hali hiyo, wawakilishi hao kupitia kwa Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga, wameapa kucheza kwa nguvu zote, kuhakikisha wanashinda mchezo huo na hatimaye kusonga mbele.
“Tunashukuru tumefika salama, lakini kwa bahati mbaya tumekutana na baridi kali sana…hata hivyo hali hii isiwatie hofu Wanayanga, kuwa timu yetu itashindwa kuhimili mikikimikiki ya huku,” alisema Nchunga katika mahojiano yake na mtandao mmoja wa nchini Misri.
Katika mchezo wa leo, Yanga huenda ikawakilishwa na Shaban Kado, Nahodha Shadrack Nsajigwa, Stefano Mwasyika,  Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Omega Seme, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah na Davies Mwape.
Pia nyota wengine wa Yanga walio huko ni pamoja na Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Shamte Ally, Jerry Tegete, Pius Kisambale, Oscar Joshua na Job Ibrahim, ambao wote wako fiti.
Yanga inayonolewa na Mserbia, Kostadin Papic, inatakiwa kucheza kwa umakini mkubwa kutokana na wapinzani wao kuwa na nyota wengi wenye uzoefu na uwezo mkubwa.
Yanga inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 kuitoa Zamalek kwenye michuano hiyo ambapo katika mchezo wa awali uliopigwa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Yanga haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri tangu ianze kukutana nazo mwaka 1982.
Mafanikio makubwa kwa Yanga katika michuano ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 na wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika, walicheza robo fainali mara mbili 1969 na 1970 na pia Robo Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1996.

Comments