WENGER ATAMBA, ARSENAL ITACHEZA LIGI YA MABINGWA MSIMU UJAO

KOCHA wa Arsenal Arsene Wenger ana matumaini kuwa ushirikiano ulioonyeshwa na wachezaji licha ya wao kushindwa na AC Milan utawapa nguvu ya kurudi kwenye ligi ya klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao.
Arsenal waliwafunga Milan 3-0 katika raundi ya pili ya timu 16 zilizobaki lakini wakashindwa kwa matokeo ya jumla 4-3.
Kumaliza katika nafasi nne za kwanza kwenye ligi kuu ya England ndio lengo la Wenger sasa, aliyesema: "Ni jambo la kusikitisha kwa wachezaji lakini timu hii imekuwa na ushirikiano mzuri.
"Natarajia kwamba kutoka hapa tutamaliza msimu vizuri."
Ikiwa imebaki mechi 11 kabla ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu ya England, Arsenal iko katika nafasi ya nne baada ya kuwafunga Tottenham walio katika nafasi ya tatu na Liverpool ambao wako katika nafasi ya saba kwenye mechi zao mbili za mwisho.
"Tunajua tunatakiwa tujitahidi zaidi kwenye ligi," Alisema Wenger. "Kwetu sisi kila pointi lazima tuipiganie na hadi mwisho wa msimu,hilo ndilo lililoko mbele yetu kwa sasa.
" Cha msingi lengo letu linawezekana kutimia kwa sababu tuna pointi nne nyuma ya Tottenham. Tunatakiwa tuende hatua kwa hatua. Tuna mechi nyingine kubwa Jumatatu usiku dhidi ya Newcastle.
" Kwetu sisi ni wazi - lazima tushinde mechi zetu."
Wachezaji wa Arsenal watakuwa na matumaini zaidi sasa baada ya ushindi katika mechi zao tatu zilizopita kwa ujumla.

Comments