VITA VPL YAHAMIA MORO UNITED, VILLA


Timu za Moro United na Villa Squad ambazo ziko kwenye vita ya kukwepa kushuka daraja katika Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinapambana kesho (Machi 28 mwaka huu) kwenye moja kati ya mechi mbili za siku hiyo.
 
Mechi hiyo namba 153 itachezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili. Moro United iko nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18 wakati Villa Squad iko nafasi ya 14 kwa pointi zake 14.
 
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 kwa jukwaa kuu. Mwamuzi atakuwa Andrew Shamba akisaidiwa na Samson Kobe na Idd Mikongoti wote wa Dar es Salaam.
 
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Arthur Mambeta wa Dar es Salaam wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Emmanuel Chaula kutoka mkoani Rukwa.
 
Mechi nyingine ya Machi 28 mwaka huu itakayochezeshwa na mwamuzi Judith Gamba wa Arusha itakuwa kati ya Ruvu Shooting itakayoikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
 
Gamba katika mechi hiyo namba 150 atasaidiwa na Saada Tibabimale kutoka Mwanza na Hellen Mduma wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba ni Juma Safisha wa Pwani wakati Kamishna ni Hamis Kissiwa wa Dar es Salaam.
 
Mechi za Machi 31 mwaka huu ni Coastal Union dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi ya African Lyon na Simba.
 
RHINO, POLISI DAR KUANZA FAINALI FDL
Timu za Rhino Rangers ya Tabora na Polisi Dar es Salaam zitapambana Machi 31 mwaka huu katika moja ya mechi za ufunguzi wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza zitakazochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
 
Kila siku zitachezwa mechi mbili, moja ikianza saa 8 mchana wakati ya pili ni saa 10 jioni ambapo fainali hiyo itamalizika Aprili 22 mwaka huu kwa timu tatu za kwanza kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao- 2012/2013.
 
Morogoro imepewa uenyeji baada ya kulipa sh. milioni 20.5 kati ya sh. milioni 25 zilizotakiwa. Sh. milioni 4.5 zilizobakia imekubaliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa itazilipa moja kwa moja kwenye huduma zitakazotumiwa na wasimamizi wa fainali hizo.
 
Mkoa mwingine ulioomba uenyeji ulikuwa Mbeya. Lakini wenyewe hadi Machi 26 mwaka huu ambayo ilikuwa siku ya mwisho kufanya malipo ulikuwa umeingiza kwenye akaunti ya TFF sh. milioni 15.
 
Upangaji ratiba (draw) ulifanyika jana (Machi 26 mwaka huu) kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kushuhudiwa na viongozi wa timu saba kati ya tisa zinazocheza fainali hizo.
 
Mechi ya pili siku ya ufunguzi itakuwa kati ya Trans Camp na Mbeya City Council. Aprili Mosi ni Tanzania Prisons na Polisi Morogoro zitakazocheza mchana wakati jioni ni Mgambo Shooting na Mlale JKT.
 
Aprili 2 mwaka huu ni Polisi Tabora vs Rhino Rangers (mchana) na Polisi Dar es Salaam vs Trans Camp (jioni). Aprili 3 mwaka huu ni Mbeya City Council vs Tanzania Prisons (mchana) na Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (jioni).
 
Aprili 5 mwaka huu ni Polisi Tabora vs Mlale JKT (mchana) wakati jioni ni Rhino Rangers vs Trans Camp. Aprili 6 mwaka huu Polisi Dar es Salaam vs Mbeya City Council (mchana) wakati jioni ni Tanzania Prisons vs Mgambo Shooting.
 
April 8 mwaka huu ni Mlale JKT vs Polisi Morogoro (mchana) wakati jioni itakuwa Polisi Tabora vs Polisi Dar es Salaam. Aprili 9 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Rhino Rangers (mchana) wakati jioni ni Trans Camp vs Tanzania Prisons.
 
Aprili 11 mwaka huu ni Mbeya City Council vs Polisi Tabora (mchana) na Mlale JKT vs Rhino Rangers (jioni). Aprili 12 mwaka huu Polisi Dar es Salaam vs Mgambo Shooting (mchana) na Polisi Morogoro vs Trans Camp (jioni).
 

Comments