VILLA SQUAD YAAPA KUTOSHUKA DARAJA


TIMU ya Villa Squad ya Magomeni Dar es Salaam, inayoburuza mkia katika Ligi kuu ya soka Tanzania bara imejitapa kuwa bado inayo matumaini ya kujinusuru na janga la kushuka daraja.
 Katibu Mkuu wa muda wa Villa, Frank Mchaki, alisema kuwa wanaamini watakuwa kati ya timu zitakazobaki na kucheza Ligi kuu mwakani licha ya kuwa mkiani.
Mchaki alisema wanaamini hivyo kutokana na molari walionao wachezaji wao hivi sasa ambapo wanaamini watashinda mechi zao zote sita zilizosalia za Ligi kuu.
Alisema kuwa tayari wameyafanyia masahihisho makosa yaliyojitokeza katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga ambayo walipoteza dakika ya mwisho ya mchezo huo.
“Sisi Villa Squad tunapenda kuwaambia wana Kinondoni kuwa waendelee kutuunga mkono tunawahakikishia kuwa tutabaki Ligi kuu, wasifikirie kabisa suala la kushuka daraja,” alisema Machaki.
Alisema kwa pointi 16 walizonazo iwapo watashinda zote na timu zilizo juu yake za Polisi Dodoma yenye pointi 17 na michezo minne mkononi, Moro Dodoma yenye pointi 18 na michezo sita mkononi na African Lyon yenye pointi 18 na michezo saba mkononi ndizo zitakazoshuka.
Aliongeza kuwa wachezaji wao wanaoendelea kujifua kwa nguvu zote wameahidi kufia uwanjani kuhakikisha wanashinda mechi zote ili timu hiyo iweze kubaki Ligi kuu msimu ujao.

Comments