TIBAIGANA AWAPA ONYO KALI RAGE, SENDEU




Kikao cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, iliyoketi kusikikiza mashitaka dhidi ya Alhaj Ismail Aden Rage na Louis Sendeu kilifanyika leo tarehe 24 Machi, 2012 kilisikiliza tuhuma zilizowasilishwa na TFF. Mashitaka hayo yalihusiana na matamko yaliyotolewa na watuhumiwa hao kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga, uliochezwa tarehe 17 Agosti, 2011.
Katika mashitaka hayo, watuhumiwa hao walituhumiwa kukiuka Kanuni ya 30 (1) (f) na Kanuni ya 53 (1) (2) cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutafakari maelezo hayo, pamoja na kuchambua sheria na kanuni mbalimbali, Kamati imeamua yafuatayo:
Hasara kwa Mdhamini
Kuhusiana na suala hasara, Kamati inaona kwamba suala hili halikuwa na uzito wowote  wala hakukuwa na hoja ya msingi, wala ushahidi wa kuthibitisha kwamba tishio au matamko hayo yalikuwa na uhusiano na hasara inayodaiwa kwamba mdhamini huyo aliipata. Hakuna malalamiko yoyote yaliyotolewa kuhusiana na kinachodaiwa kuwa ni hasara inayotokana na matamko ya viongozi hawa. Kamati imeitupilia mbali hoja hii.

Tuhuma za matamko ya watuhumiwa
Kamati imebaini kwamba matamko hayo yalikuwa ni uvunjaji wa kanuni na yalilenga kuchochea hisia mbaya na kuleta vurugu. Kamati ina maoni ya kwamba viongozi wa vilabu hivi walistahili kufuata taratibu za kawaida katika kudai haki zao, badala ya kutoa matamko ambayo yangeweza kuchochea  hisia mbaya. Kitendo hicho si cha kiungwana na kinaendana kinyume na taratibu za uongozi wa mpira.
Wao kama viongozi, walistahili kutumia utashi na kupima athari za matamko yao, ili kuepuka uwezekano wa kuleta msuguano usio wa lazima na kuungiza mchezo wa mpira katika kashfa au kukosa heshima. Matamko haya yanaweza kuwa ni kichocheo kwa viongozi wengine wenye tabia ya namna hiyo kutumia mwanya huu kufanya vitendo hivyo.
Kwa msingi huo, Kamati inawaona wote wawili kuwa wana hatia na matamko hayo yanayohusiana na mchezo huo. Kwa kuzingatia hilo, Kamati inatoa onyo kali dhidi ya watuhumiwa hao wawili na inaonya kwamba adhabu kali zaidi zitachukuliwa kama watuhumiwa watalirudia kosa kama hili au linalofanana na hilo.
Kamati imebaini pia kwamba Mheshimiwa Aden Rage amehusika pia na kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Bwana Saad Kawemba wa TFF, akidaiwa kwamba alikuwa anazuia usajili wa mchezaji Gervais Kago na kwamba Bwana Kawemba alifanya hivyo kwa vile ana mapenzi na klabu ya  pinzani ya Yanga.

Pamoja na kwamba hakukuwa na athari za moja kwa moja dhidi ya Bwana Kawemba, ukweli ni kwamba kitendo hicho kilikuwa ni kosa ambalo halistahili kufanywa na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi kama Mheshimiwa Rage, na kilikuwa kina dalili za kuchochea chuki zisizo na msingi dhidi ya Bwana Kawemba. Kitendo hicho kilikuwa kinakiuka kifungu cha 53 (1) (2) cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Kamati inatoa onyo kali dhidi ya Mheshimiwa Aden Rage kwa kupatikana na hatia yake hiyo.

Imetolewa na Kamati ya Nidhamu na usuluhishi leo tarehe 24 Machi, 2012.

..................................................
Kamishna Alfred Tibaigana
Mwenyekiti wa Kamati

Comments