TFF YAJIKANUSHA UENYEJI DARAJA LA KWANZA





SIKU moja baada ya Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura kutangaza kwa Mkoa wa Morogoro ndio uliopewa uenyeji wa fainali za Ligi daraja la Kwanza mwaka huu  TFF imekanusha taarifa hiyo. 
Kaimu Katibu Mkuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni (pichani), amesema kuwa  Chama cha Soka cha Mkoa wa Morogoro, (MRFA), hakijapewa uenyeji bali kinayo nafasi kubwa ya kushinda uenyeji huo.
Kayuni alisema kuwa, usahihi ni kwamba Morogoro ina nafasi kubwa kwa vile ndiyo pekee iliyotoa kiasi cha sh mil 10,000 kati ya sh mil 25,000 ambazo zilikuwa moja ya masharti anayopaswa kuyatekeleza mwombaji wa nafasi ya uenyeji wa fainali hizo.
Alisema kutokana na hilo Mkoa huo umepewa hadi Machi 25 kumalizia kiasi cha fedha kilichosalia na iwapo itashindwa kamati ya Ligi itakayoketi Machi 26 inaweza kutoa uamuzi wa kuinyang’anya nafasi hiyo.
“TFF tunapenda kusahihisha taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari kwamba Morogoro imepewa uenyeji wa fainali za Ligi daraja la kwanza, usahihi ni kuwa Morogoro haijapewa nafasi hiyo bali inayo nafasi kubwa ya kupewa uenyeji huo kwa sababu imelipa kiasi kikubwa cha fedha, ambazo ni moja ya masharti ya kuomba uenyeji,” alisema Kayuni.
Alisema kuwa Mikoa mingine iliyoomba kupewa uenyeji huo licha ya kukumbushwa mara kwa mara lakini haikuonyesha utayari kwani hakuna Mkoa uliolipa japo sehemu ya fedha hizo sh ml 25.
Timu zinazotarajiwa kushiriki fainali hizo hiyo kutoka kundi A ni Polisi Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga na Transit Camp ya Dar es Salaam, Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma na Tanzania Prisons ya Mbeya wakati C ni Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.


Comments