SIMBA, YANGA ZASAKA POINTI VPL KESHO

Yanga na Simba ni miongoni mwa timu nne zitakazokuwa viwanjani kesho (Machi 31 mwaka huu) kusaka pointi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo iko katika raundi ya 22.
 
Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi namba 148 kati ya Coastal Union na Yanga. Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma ambaye atasaidiwa na Rashid Lwena (Ruvuma) na Issa Malimali (Ruvuma).
Mwamuzi Amon Paul wa Musoma ndiye atakayechezesha mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio kwenye mechi ya African Lyon na Simba ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 15,000.
Aprili Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi ya VPL kati ya Azam na Ruvu JKT itakayochezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 jukwaa kuu.

Comments