SIMBA WALEEE, AZAM WAITEREMSHA YANGA


MABAO ya ‘ma tx’ kiungo wa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango dakika ya 18 na mshambuliaji wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya 74,  jioni ya leo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro yameiwezesha Simba SC kukalia kwa madaha- kwa kujinafasi kiti cha uongozi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuibwaga Mtibwa Sugar 2-1.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Hussein Omar Javu aliifungia Mtibwa bao lililokuwa la kusawazisha dakika ya 52, ambalo mwisho wa mchezo lilikuwa la kufutia machozi- kufuatia Sunzu kutupia la ushindi kwa Simba.
Ushindi huo, unawafanya Wekundu wa Msimbazi watimize pointi 47- wakiwaacha kwa pointi nne mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 43 katika nafasi ya tatu.
Azam jana ilirudi nafasi ya pili kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Mbagala jioni ya leo, bao pekee la Mrisho Khalfan Ngassa.
Ushindi huo, unaifanya Azam sasa itemize pointi 44, ingawa imecheza mechi moja zaidi ya mabingwa watetezi, wakati Simba nayo pia imecheza mechi moja zaidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga.

Comments