SIMBA HAINA PRESHA NA WALGERIA


Na Dina Ismail
KLABU ya soka ya Simba imesema haina haja ya kwenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya Algeria, imefahamika.
 
Simba imevuka hatua hiyo baada ya kuisukumiza nje ya michuano hiyo Kiyovu Sport ya Rwanda hivyo itakwaana na  Wa Algeria hao mwishoni mwa wiki ijayo.
 
Akizungumza kwa simu jana Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Rage alisema kwamba wameona hakuna haja ya kwenda kujinoa nje ya nchi kutokana na hali ya hewa ya Algeria kuwa sawa na ya hapa nchini.
 
Alisema pamoja na hali ya hewa wamebaini kuwa wapinzani wao si timu ya kutisha sana hivyo wameona waendelea kujinoa hapa nchini kupitia michezo ya ligi kuu soka Tanzania Bara inayoendelea kwa sasa.
 
“Maandalizi ya Algeria yanakwenda vema ingawa hayatupi presha kubwa sana kwa kuwa tumeshazipata taarifa zao kwa kiasi kikubwa na mwalimu anazifanyia kazi...lakini suala la kambi litaendelea kuwa hapa nchini na huko tutaenda siku chache kabla ya mchezo,”Alisema Rage.
 
Katika hatua nyingine, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka mjini Dodoma leo kwenda Morogoro tayari kwa mchezo wake wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa keshokutwa katika katika dimba la Jamhuri. 

Comments