SERIKALI YAICHACHAMALIA TFF, SASA MIL.10 KWA UHARIBIFU WOWOTE TAIFA




KUANZIA sasa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) litawajibika kulipa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa uharibifu wa idadi yoyote ya viti utakofanywa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .   
Hatua hiyo inafuatia kukithiri kwa uharibifu wa viti hivyo ambao umekuwa ukifanywa na mashabiki wa soka hapa nchini na hasa wa Vilabu vya Simba na Yanga.   
Akizungumza jana kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini Leonard Thadeo alisema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti vitendo vya uharibifu wa viti katika Uwanja huo. 
Alisema fedha hizo zitalipwa bila kujali idadi ya viti hata kiwe kimoja au kumi kwani serikali imesikitishwa na kitendo cha muendelezo wa vurugu kwenye uwanja huo kwani kinawadhalilisha wanamichezo wote wa Tanzania na jumuiya ya Kimataifa. 
Thadeo aliongeza kuwa uharibifu huo umekuwa ukifanyika mara kwa mara na serikali imekuwa ikilazimika kufanya matengenezo bila kuwahusisha wadau wengine lakini inaonekana kujengeka kuwa tabia miongoni mwa baadhi ya mashabiki hatua ambayo haiwezi kuvumilika. 
“Inasikitisha kuona hata baadhi ya viongozi wa vilabu vyetu hawatambui kuwa wanawajibu wa msingi kama viongozi kuwaelimisha wanachama  na wapenzi wa vilabu vyao kuacha uharibifu badala yake wanadai kuwa viti vingi viliharibika,kaharibu nani? alihoji Thadeo. 

Comments